Benki ya Dunia: Maskini hohehahe wamepungua

Watoto Haki miliki ya picha Getty
Image caption Karibu nusu ya watu maskini duniani bado watakuwa wakiishi Afrika kusini mwa Sahara

Benki ya Dunia imesema kwa mara ya kwanza kabisa chini ya asilimia 10 ya watu duniani watakuwa wakiishi katika umaskini uliokithiri kufikia mwisho wa mwaka 2015.

Benki hiyo imesema pia kuwa inatumia kiwango kipya cha mapato cha $1.90 kila siku kubaini wanaoishi katika umaskini uliokithiri, kikiongezeka kutoka mapato ya $1.25 kila siku.

Inakadiria kuwa watu walio katika umaskini uliokithiri duniani watashuka kutoka 12.8% mwaka 2012 hadi 9.6%.

Hata hivyo, watu maskini zaidi bado wanapatikana Afrika kusini mwa jangwa la Sahara.

Ingawa watu maskini eneo hilo watashuka kutoka 42.6% mwaka 2012 hadi 35.2% kufikia mwisho wa 2015, bado watakuwa karibu nusu ya maskini wote duniani.

"Hiki ndicho kizazi cha kwanza kabisa katika historia kinachoweza kumaliza umaskini uliokithiri,” rais wa Benki ya Dunia Jim Yong Kim amesema.

Benki hiyo imesema kushuka kwa idadi ya watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri kumetokana na ukuaji wa kiuchumi katika mataifa yanayoendelea na uwekezaji katika elimu, afya na huduma za kijamii.

Lakini Bw Kim alionya kuwa itakuwa vigumu kupiga hatua zaidi ikizingatiwa kupungua kwa kasi ya ukuaji wa kiuchumi duniani, mizozo, misukosuko masoko ya kifedha, ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

Benki hiyo pia imeonga kuwa umaskini “unazidi kukita mizizi katika mataifa yanayokabiliwa na mizozo na yanayotegemea sana uuzaji wa bidhaa ghafi nje.”