Shule zafunguliwa tena Kenya

Wanafunzi Kenya
Image caption Walimu walirejea kazini bila kuwepo makubaliano yoyote kuhusu nyongeza ya mishahara

Shule nchini Kenya zimefunguliwa tena baada ya walimu kusitisha mgomo wao uliokuwa umedumu kwa wiki tano.

Vyama viwili vinavyotetea walimu nchini humo vilitangaza mwishoni mwa wiki kwamba zitatii agizo la mahakama la kuwataka walimu warudi shuleni.

Walimu takriban 280,000 walikuwa wamegoma kuishinikiza serikali iwalipe nyongeza ya mishahara ya asilimia 50 hadi 60.

Lakini mahakama ya masuala ya mizozo ya kiviwanda na masuala ya wafanyakazi iliwaamuru warudi kazini na kamati huru ya kuongoza mazungumzo kati yao na serikali iundwe.

Kamati hiyo inafaa kuwa imepata suluhu katika muda wa siku 90.

Akitangaza kusitishwa kwa mgomo, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu Kenya Wilson Sossion alisema watarejelea mgomo huo baada ya siku 90 iwapo serikali haitatimiza ahadi ya kuwalipa nyongeza hiyo ya mishahara.