Marekani yalaumu Afghanistan kwa shambulio Kunduz

MSF Haki miliki ya picha AFP
Image caption Shirika hilo linasema haikubaliki kushambulia hospitali

Jenerali mmoja mkuu wa jeshi la Marekani amesema wanajeshi wa Afghanistan ndio walioomba majeshi ya taifa hilo yashambulie kliniki iliyokuwa ikitumiwa na shirika la madaktari wasio na mipaka la Medecins Sans Frontieres (MSF) mjini Kunduz.

Shambulio hilo la ndege liliua watu 22.

Jenerali John Campbell alikiri kuwa wanajeshi wa Marekani hawakuwa wameshambuliwa kufikia wakati huo.

MSF imesema juhudi za Afghanistan kutana kuonyesha shambulio hilo lilikuwa la haki ni “kukiri kosa la uhalifu wa kivita”.

Wanajeshi wa Afghanistan wakisaidiwa na wenzao wa Marekani wamefanikiwa kukomboa maeneo mengi ya Kunduz, mji uliokuwa umetekwa na wapiganaji wa Taliban wiki iliyopita.

Wafanyakazi 12 wa MSF na wagonjwa 10 walifariki kwenye shambulio hilo lililotekelezwa na Marekani.

Shirika la MSF linasema hospitali hiyo ilikuwa ikitegemewa sana na maelfu ya wakazi wa jiji hilo na maeneo mengine ya Afghanistan kaskazini.

"Tumefahamu sasa kwamba mnamo Oktoba 3, wanajeshi wa Afghanistan walisema walikuwa wakishambuliwa na adui na wakaomba usaidizi wa angani kutoka kwa wanajeshi wa Marekani,” alisema Jenerali Campbell, ambaye ni kamanda mkuu wa majeshi ya shirika la kujihami la Nato yanayoongozwa na Marekani ambayo yanahudumu Afghanistan.

“Shambulio la kutoka angani lilihitajika kuangamiza hatari ya Taliban na raia walishambuliwa kimakosa,” alisema.

Aliomba radhi kutokana na vifo hivyo vya raia.

Akijibu matamshi hayo ya Jenerali Campbell, mkurugenzi mkuu wa MSF Christopher Stokes, ameituhumu Marekani kwa “kujaribu kupitisha lawama kwa serikali ya Afghanistan”.

“Ukweli ni kwamba Marekani ndio walioangusha mabomu hayo,” Bw Stokes alisema.

“Marekani walishambulia hospitali kubwa iliyojaa majeruhi na wafanyakazi wa MSF.”