Wapiganaji wa Houthi wakubali mpango wa UN

Houthi Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mashauriano ya kumaliza vita Yemen yanafanikishwa na UN

Wapiganaji wa Houthi nchini Yemen wamethibitisha kujitolea kwao kuunga mkono mpango wa amani uliopendekezwa na Umoja wa Mataifa.

Kupitia barua ambayo BBC imefanikiwa kuiona, wawakilishi wa Houthi wameahidi kutekeleza mpango wa amani wenye mambo saba muhimu.

Mpango huo uliafikiwa baada ya mazungumzo yaliyofanikishwa na Umoja wa Mataifa mjini Muscat, Oman.

Barua hiyo iliyotumwa kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon imefuatia tangazo lisilo rasmi lililofanywa na wapiganaji hao mwezi jana wakiahidi kuunga mkono maazimio hayo.

Umoja wa Mataifa unasema karibu watu 4,900 wameuawa katika mapigano nchini Yemen, 2,355 kati yao wakiwa raia.

Kwenye barua hiyo, wapiganaji hao wanaahidi kuunga mkono maazimio saba kutoka Muscat, ambayo ni kusitisha mapigano, kuondoa wapiganaji mijini na kurejea kwa serikali mji mkuu Sanaa.

Rais wa Yemen Abdrabbuh Mansour Hadi amesisitiza kuwa sharti wapiganaji wa Houthi waondoke maeneo waliyoteka kabla ya mkataba wa Amani kutiwa saini.

Wawakilishi wa Houthi, wanaojulikana rasmi kama Ansar Allah, wanataja mpango huo wa amani kuwa "shughuli muhimu …katika kurejelewa kwa mchakato wa kisiasa.”

"Kutoka upande wetu, tunajitolea kuunga mkono mambo hayo saba kama kiungo moja,” wanaongeza kwenye barua hiyo.

“Tunakaribisha wito wa UN kwa pande zote kurejea kwenye meza ya mazungumzo.”

Barua hiyo inakosoa serikali, ikidai haijaonyesha nia yoyote ya kuunga mkono mpango huo wa Umoja wa Mataifa.