Murdoch asema Obama si ‘rais mweusi kamili’

Obama Haki miliki ya picha AFP
Image caption Obama amekuwa mwangalifu sana kuhusu masuala ya rangi wakati wa utawala wake

Tajiri wa vyombo vya habari duniani Rupert Murdoch ameandika ujumbe kwenye Twitter akidokeza kwamba Rais Barack Obama si "rais mweusi kamili”.

Kwenye ujumbe wa kumsifu mmoja wa wanaotaka kuwania urais Marekani kupitia chama cha Republican Ben Carson, Bw Murdoch ameandika: "Ben na Candy Carson wazuri sana. Itakuwaje tukiwa na rais mweusi kamili atakayeangazia kikamilifu masuala ya rangi? Na mengine mengi”.

Amependekeza pia watu wasome makala iliyo kwenye jarida la New York Magazine inayozungumzia “kutamaushwa kwa makundi ya wachache” na uongozi wa Rais Obama.

Bw Murdoch, 84, ndiye mwanzilishi wa himaya ya mashirika ya habari ya News Corporation iliyokita mizizi maeneo mengi duniani.

Kampuni yake inamiliki Fox News Channel, The New York Post na The Wall Street Journal nchini Marekani na magazeti ya Times nchini UIngereza miongoni mwa vyombo vingine vya habari.

Ameorodheshwa mmoja wa watu wenye ushawishi zaidi duniani.

Bw Murdoch awali alikuwa ameandika kwenye akaunti yake ya Twitter jinsi anavyofurahishwa na Bw Carson.

Mgombea huyo wa urais mwenye umri wa miaka 63 ni mtaalamu wa upasuaji wa mfumo wa neva na mmoja wa wagombea 15 wanaopigania tiketi ya chama cha Republican kuwana urais Marekani 2016.

Siku chache zilizopita, aliandika kwenye Twitter: “Kotekote, wadadisi wa masuala ya kisiasa wanamdunisha Ben Carson. Lakini umma unafahamu na kupendezwa na upole na unyenyekevu."

Haki miliki ya picha REUTERS
Image caption Murdoch ni mmoja wa watu wenye ushawishi zaidi duniani

Awali, alisema haya kumhusu: "Huenda ndiye wa kupigiwa upatu. Hana doa katika historia ya maisha yake, ufanisi, sifa zake na maono.”

Rais Obama, katika uongozi wake, amekuwa mwangalifu kuhusu masuala ya ubaguzi wa rangi na asili.

Jarida la New Yorknakala ya wiki hii linawanukuu Waafrika-Wamarekani wakisema wangelipenda afanye mengi zaidi kutatua shida za ubaguzi wa rangi.

Bw Carson aliibua utata mwezi uliopita baada ya kusema Mwislamu hafai kuwania urais Marekani kwa kuwa Uislamu unakinzana na katiba ya Marekani.