Nyota wa Suffragette atetea usawa katika filamu

Meryl Streep Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Streep amelalamikia kutengwa kwa wanawake katika uamuzi kuhusu ubora wa filamu

Mwigizaji Meryl Streep amesema ni jambo la “kuudhi sana” kwamba umaarufu wa filamu huongozwa na utathmini ambao hufanywa na watathmini ambao wengi wao huwa wanaume.

Mwigizaji huyo, aliyewahi kushinda tuzo ya Oscar, anaigiza kama mtetezi wa haki za wanawake Emmeline Pankhurst katika filamu kwa jina Suffragette.

Filamu hiyo, ambayo pia inashirikisha Carey Mulligan, ilizinduliwa katika Tamasha za Filamu za London Jumatano.

Akizungumza kabla ya sherehe kuu ya kuanza kuonyeshwa kwa filamu hiyo, Streep alilalamika kuwa wanawake wamekosa kujumuishwa katika biashara nyingi duniani.

"Iwapo wanaume huwa hawatazami wanapoketi mezani mikutano na bodi za wakurugenzi na kuhisi kuna jambo lisilioenda vyema nusu ya wanachama wakiwa si wanawake, basi hatutapiga hatua zozote,” alisema.

Akizungumzia tasnia ya filamu, Streep alisema: “Sehemu kubwa ya biashara hii huongozwa na msisimko. Nilitaka kujua nini huongoza msisimko huu.”

Alisema alihesabu idadi ya watathmini wa filamu na wanablogu walioidhinishwa kwenye tovuti mashuhuri ya Rotten Tomatoes na kugundua kuwa 168 walikuwa wanawake na 760 wanaume. Jopo la utathmini wa filamu la New York lilikuwa na wanaume 37 na wanawake wawili pekee.

"Wanaume na wanawake si sawa, wakati mwingine hutofautiana kwa vitu vinavyowapendeza. Wanapenda ladha tofauti,” alisema Streep.

"Hili hata huwezi kusema ni jambo la kuvunja moyo, ni jambo la kuudhi. Watu hukubali utathmini huu na kuamini ni wa busara … tunahitaji jinsia zote zijumuishwe.”

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Streep amesema wanawake na wanaume hupendezwa na mambo tofauti

Hayo yakijiri, wanaharakati wanaotetea watu wanaopigwa na wachumba wao nyumbani walifyatua fataki za kutoa moshi na kujilaza kwenye zulia jekundu wakati wa kuanza kwa tamasha hizo uwanja wa Leicester.

Waandamanaji hao walibeba mabango yenye maandishi “majeraha huua” na “wanawake marehemu hawawezi kupiga kura”.