Brazil, Argentina zashindwa mechi za kufuzu Kombe la Dunia

Brazil team Haki miliki ya picha EPA
Image caption Brazil imeshindwa kutamba tangu ikose kufana katika Kombe la Dunia mwaka jana

Mataifa mawili yanayojulikana sana kwa kusakata gozi Amerika Kusini yalicharazwa kwenye mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia zilizochezwa Alhamisi.

Brazil waliokuwa wakicheza bila nyota wao anayechezea Barcelona Neymar, walilazwa 2-0 ugenini Chile mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia Urusi 2018.

Mambo yalikuwa sawa kwa Argentina waliokubali kichapo cha 2-0 nyumbani kutoka kwa Ecuador, wakicheza bila nyota wao wa Barcelona Lionel Messi.

Chile walishinda kupitia mabao mawili ya kipindi cha pili kutoka kwa Eduardo Vargas na Alexis Sanchez.

Neymar anatumikia marufuku ya mechi mbili za mwisho kati ya nne alizosimamishwa kucheza miezi mitatu iliyopita wakati wa Copa America. Pia atakosa mechi ya wiki ijayo dhidi ya Venezuela.

Mjini Buenos Aires, miamba wa soka Argentina, walikubali kupokea mabao mawili kipindi cha pili kutoka kwa Frickson Erazo na Felipe Caicedo wa Ecuador.

Nyota wao Messi anauguza jeraha la goti na anatarajiwa kurejea uwanjani mwishoni mwa Novemba.

Argentina hata hivyo walikuwa na nyota wengi uwanjani, wakiwemo Angel Di Maria, Sergio Aguero and Javier Macherano.

Kwneye mechi nyingine za kufuzu Alhamisi, Uruguay walilaza Bolivia 2-0 mjini La Paz kupitia Martin Caceres na Diego Godin.

Uruguay walishinda bila Luis Suarez na Edinson Cavani.

Paraguay nao walilaza Venezuela 1-0, bao hilo pekee la mechi hiyo likitoka kwa Derlis Gonzalez dakika ya 84.