Wakazi wajawa na wasiwasi kuhusu El Nino Kenya

El Nino Kenya
Image caption Serikali imekuwa ikijikakamua kuzibua na kukarabati mitaro na mabomba ya kupitishia maji

Mvua imeanza kunyesha maeneo mengi Kenya na wataalamu wa utabiri wa hali ya hewa wanasema mvua kubwa ya El Nino itanyesha na huenda ikasababisha madhara makubwa.

Mara ya mwisho mvua ya El Nino kunyesha Kenya mwaka 1997 ilisababisha vifo vya watu na mifugo pamoja na kuharibu mali na miundo msingi.

Wakazi wa maeneo ambayo huathiriwa na mafuriko wameingiwa na wasiwasi ingawa wengi wanasema hawana la kufanya.

Wakazi wa kijiji cha Mukuru kwa Njenga jijini Nairobi, wanasema wanatarajia eneo hilo kuathirika pakubwa iwapo mvua hiyo itanyesha.

Shule ya upili ya Embakasi ambayo imo katika eneo hilo imegeuzwa kuwa ya msimu kwani hufungwa kila mvua kubwa inaponyesha.

Mwaka huu shule hiyo iimefungwa mara mbili kwa sababu maji hujaa katika mabweni ya wanafunzi pamoja na madarasa. Walimu wana wasiwasi matokeo ya wanafunzi katika mitihani yataathiriwa na mvua hiyo.

Image caption Idara ya utabiri wa hewa Kenya imesema maeneo mengi yatapokea mvua kubwa isiyo ya kawaida

Mjini Narok, kilomita 147, kutoka jiji kuu la Nairobi, hali ni hiyo hiyo.

Walter Ngoju ambaye ni mfanyibiashara katika mji huo anasema alimpoteza mkewe pamoja na mali ya mamilioni ya pesa mvua kubwa iliponyesha mapema mwaka huu.

"Mvua ikinyesha hapa huwa nafunga biashara na kujiendea zangu. Mwezi Aprili mvua kubwa ilinyesha na ikasomba mali yangu yote pamoja na mke wangu," ameambia mwandishi wa BBC Hawa Khala.

Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya, maeneo mengi ya magharibi mwa Kenya na pwani tayari yanapokea mvua kubwa.

Image caption Mji wa Narok huathiriwa sana mvua inaponyesha

Maeneo mengine kama Narok yanashuhudia upepo mkali na mawingi mazito yanatanda.

Maafa pekee yaliyoripotiwa ni vifo vya watu wanne eneo la Kithurine, Meru kusini karibu na Mlima Kenya katika chimbo la mawe.

Mkurugenzi wa shirika la kukabiliana na majanga nchini Kenya Nathan Kigotho anasema Serikali iko tayari kukabiliana na dharura mvua ya El Nino ikinyesha.

"Tunajua maji mengi yatakuja na magonjwa kutokea na wizara ya afya imejiandaa. Kadhalika, sehemu ambazo huwa zinaathiriwa na mvua ya kawaida huko tumepeleka chakula na dawa wakati huu kabla mvua haijaanza kunyesha,” anasema.

"Pia, tumezibua njia za kupitishia maji ili kupunguza mafuriko."