Uturuki yaomboleza vifo vya watu 95

Haki miliki ya picha epa
Image caption Waombolezaji nchini Uturuki wakati wa mazishi

Maelfu ya Watu wamekusanyika mjini Ankara nchini Uturuki kuomboleza kwa ajili ya Watu takriban 95 waliouawa kwa milipuko miwili ya mabomu.

Watu wanaounga mkono Chama cha Kikurdi ambao walikuwepo kwenye mkutano katika eneo ambalo mabomu yalilipuka wanaamini kuwa idadi ya kweli ya waliopoteza maisha ni Watu 128.

Vyanzo vya ulinzi vinasema kuwa vinashuku kundi la wanamgambo wa IS kuhusika kwenye shambulio hilo.

Serikali imekana vikali madai kuwa imehusika katika mashambulizi hayo.

Milipuko ya mabomu ilitokea karibu na kituo cha treni cha mjini Ankara wakati watu walipokusanyika kwa ajili ya matembezi yaliyoandaliwa na makundi ya mrengo wa kushoto yakishinikiza kukoma kwa mapigano kati ya Serikali ya Uturuki na wanamgambo wa kikurdi.

Katika hali iliyotarajiwa, wanamgambo wa PKK walitangaza kuweka silaha chini siku ya jumamosi, wakitoa wito kwa wapiganaji wake kuachana na mapigano ya msituni nchini Uturuki , isipokuwa ikiwa ni kwa ajili ya kujilinda.

Hata hivyo,siku ya jumapili Jeshi la nchi hiyo lilisema limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo hao, likishambulia kusini mashariki mwa Utturuki na katika ngome za PKK kaskazini mwa Iraq na kuua watu 49.