Upinzani wakataa matokeo ya uchaguzi Guinea

Cellou Dalein Diallo Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kiongozi mkuu wa upinzani amedai kulikuwa na udanganyifu

Chama kikuu cha upinzani nchini Guinea kimesema hakitakubali matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Jumapili, shirika la habari la AFP linaripoti.

Chama hicho cha Union for the Democratic Forces kilikuwa awali kimesema kupitia taarifa kwamba masanduku ya kupigia kura yalikuwa yamejazwa kura na maafisa wa serikali.

Wanajeshi walipiga kura kwa kuwakilishwa na vikosi vya usalama vilifurusha maafisa wa kuhesabu kura katika baadhi ya maeneo.

"Hatuwezi kukubali matokeo ya uchaguzi huu, tunaomba yafutiliwe mbali,” kiongozi wa chama hicho Cellou Dalein Diallo amesema, akiongea kwa niaba ya wagombea wote saba wa upinzani.

"Hatutasalimu amri, tuna haki ya kueleza upinzani wetu,” aliongeza.

Matokeo hayo bado hayajatangazwa.

Vurugu zilikuwa zimetokea katika mji mkuu Conakry kabla ya uchaguzi ingawa baadaye hali ilitulia.

Rais Alpha Conde alikuwa akiwania kuongoza taifa hilo kwa muhula wa tatu.