Wanajeshi watano wa Nato wafariki Afghanistan

Puma Mk2 Haki miliki ya picha PA
Image caption Ajali hiyo ilihusisha helikopta ya kijeshi aina ya Puma Mk2

Watu watano, wakiwemo wanajeshi wawili wa jeshi la angani la Uingereza, wamefariki baada ya helikopta kuanguka Afghanistan.

Helikopta hiyo aina ya Puma Mk2 ilianguka ilipokuwa ikitua katika makao makuu ya wanajeshi wa Nato mjini Kabul. Muungano huo wa kujihami haujaeleza uraia wa watu hao wengine waliofariki wala watano waliojeruhiwa.

Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Uingereza alisema kuanguka kwa ndege hiyo kulitokana na “ajali na waa si shambulio kutoka kwa wapiganaji (wa Taliban)”

Jamaa za wanajeshi wa Uingereza waliofariki zimefahamishwa, wizara hiyo ilisema.

Familia hizo zimeomba muda kidogo kabla ya majina ya wahasiriwa hao kutangazwa.

Ajali hiyo imetokea baada ya msafara wa magari ya kijeshi ya Uingereza kushambuliwa katika mji wa Kabul, Jumapili asubuhi.

Watu saba walijeruhiwa, lakini hakuna aliyefariki.

Wizara ya ulinzi ya Uingereza imesema bomu la kutegwa lilisababisha ajali hiyo, lakini maafisa walio Kabul walisema lilikuwa shambulio la kujitoa mhanga.

Wapiganaji wa Taliban walisema walitekeleza shambulio hilo kulipiza kisasi mashambulio ya angani yaliyotekelezwa na wanajeshi wa Marekani walio kwenye muungano wa Nato eneo la Kunduz. Mashambulio hayo kwenye hospitali ya shirika la madaktari wasio na mipaka MSF liliua raia na madaktari.