Putin atetea mashambulio ya Urusi Syria

Vladimir Putiin Haki miliki ya picha EPA
Image caption Putin amesema magaidi wakiteka Syria wanaweza kuwa tishio kwa Urusi

Rais wa Urusi Vladimir Putin ametetea uamuzi wa nchi yake wa kuchukua hatua za kijeshi nchini Syria, na kusema lengo ni “kusaidia utawala halali” wa Rais wa Syria Bashar al-Assad.

Bw Putin aliambia runinga ya taifa ya Urusi kwamba Moscow pia inataka kuunda mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa maafikiano ya kisiasa.

Alikanusha madai kwamba mashambulio ya ngani ya Urusi yanalenga makundi ya upinzani badala ya wapiganaji wa Islamic State.

Wanajeshi wa Syria wamepiga hatua kubwa dhidi ya waasi wanaopinga serikali.

Wanajeshi wa Assad walipata mafanikio makubwa mikoa ya Idlib, Hama na Latakia, habari zilizothibitishwa Jumapili na maafisa mjini Damascus na pia wanaharakati wa upinzani.

Eneo kuu la vita sasa liko karibu na barabara kuu inayounganisha mji mkuu na miji mingine mikubwa, ukiwemo Aleppo, na wanajeshi wa Assad wanaaminika kulenga kufungia njia na kuzingira waasi Idlib.

Kwenye mahojiano ya Rossiya One TV Jumapili, Rais Putin amesema lengo lake ni “kuongeza uthabiti” kwenye serikali ya Assad.

Alisisitiza kwamba bila usaidizi wa Moscow kwa Assad, kuna hatari kwamba makundi ya kigaidi huenda yakateka na kutawala Syria.

Alieleza kwamba serikali ya Assad kwa sasa “imezingirwa” na wapiganaji walikuwa karibu sana na mji wa Damascus.

Kiongozi huyo wa Urusi pia alitoa wito kwa mataifa mengine kuungana katika kukabili “uovu wa ugaidi”.

Haki miliki ya picha Russian Defense Ministry
Image caption Urusi ilianza mashambulio ya kutoka angani Syria Septemba 30

Muungano wa majeshi unaoongozwa na Marekani, ambao umekuwa ukitekeleza mashambulio yake binafsi ya angani Syria, umesema hautashirikiana na Urusi.

Mataifa kadha, yakiwemo Uingereza na Uturuki, yametaja uungaji mkono wa Urusi kwa Assad kuwa “kosa”

Urusi ilisema Jumapili kwamba ndege zake za kijeshi lilishambulio mara 60 nchini Syria saa 24 zilizopita na kwamba ngome za IS ndizo zilizolengwa sana.

Urusi ilianza mashambulio yake Septemba 30.