Mwanamke Msomali kuavya mimba Australia

Nauru Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kisiwa cha Nauru kimekuwa kikitumiwa kuzuilia wakimbizi kabla yao kuruhusiwa kuingia Australia

Mwanamke raia wa Somalia anayedaiwa kushika mimba baada ya kubakwa katika kisiwa cha Nauru amewasili Australia kutolewa mimba hiyo.

Mwanamke huyo wa umri wa miaka 23 alikuwa ameomba ahamishwe kutoka kisiwa hicho cha Nauru wiki kadha zilizopita.

Kisiwa hicho humilikiwa na Australia na kimekuwa kikitumiwa kuzuilia watu wanaotafuta hifadhi Australia kabla yao kupewa idhini.

Mahakama kuu nchini humo kwa sasa inachunguza uhalali wa vituo hivyo vya kuzuilia wahamiaji.

Maelfu ya watu walijiunga na maandamano mwishoni mwa wiki kuunga mkono wakimbizi hao na kushinikiza serikali kufunga vituo hivyo.

Mwanamke huyo anadaiwa kuwa na mimba ya wiki 12, na anadai alibakwa na wanaume wakazi wa Nauru.

Ni haramu kuavya mimba katika kisiwa cha Nauru, ila tu maisha ya mama yanapokuwa hatarini. Ubakaji hauchukuliwi kuwa sababu tosha ya mtu kutaka kuavya mimba.

Serikali ya Australia ilikuwa awali imekabiliwa na shinikizo za kuitaka iwaruhusu wanawake kuingia nchini humo kupokea huduma za matibabu.

"Mteja wetu anaweza kupumua sasa kwamba kumekuwa na suluhu kuhusu suala hili tata,” wakili wa mwanamke huyo George Newhouse aliambia gazeti la Sydney Morning Herald.

"Kwa sasa yumo Australia na serikali ya imeamua kumpa huduma za matibabu," alisema bila kutoa maelezo zaidi.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Raia waliandamana mwishoni mwa wiki kutetea wakimbizi

Bw Newhouse alisema mteja wake ameshukuru kwa raia wa Australia kumuunga mkono na kwa maafisa wa utawala “kumuelewa”.

Lakini mwanasiasa wa upinzani amelalamikia alivyoshughulikiwa mwanamke huyo.

“Unashangaa ni kwa nini mwanamke kijana aliye katika hali ngumu ilibidi hali yake kufanywa wazi kwa umma na raia wa Australia kumsihi waziri mkuu,” alilalamika seneta wa chama cha Greens Sarah Hanson-Young, kwa mujibu wa shirika la AAP.

Hayo yakijiri, Nauru imepuuzilia mbali madai mengine ya mkimbizi mwenye asili ya Kisomali kwamba alibakwa.

Watawala katika kisiwa hicho wanasema hakuna ushahidi wa kuthibitisha madai ya mwanamke huyo kwamba alibakwa na wanaume wawili Nauru.