Taifa Stars kukutana na timu bora Afrika

Taifa Stars
Image caption Tanzania ilifuzu kwa raundi ya pili kwa kuibandua Malawi

Timu ya taifa ya Tanzania itakutana na timu iliyoorodheshwa bora zaidi Afrika kwenye raundi ijayo ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018.

Taifa Stars ilifuzu kwa raundi hiyo licha ya kulazwa na Malawi 1-0 mechi ya marudiano Jumapili kutokana na ushindi wao wa kwanza wa 2-0 jini Dar es Salaam Jumatano wiki iliyopita.

Algeria imeorodheshwa nambari 19 kwa ubora duniani kwa mujibu wa orodha ya majuzi zaidi ya Fifa. Tanzania imo nambari 136.

Harambee Stars ya Kenya nayo itakutana na Cape Verde, taifa jingine linalofanya vyema sana katika soka kwa sasa.

Timu hiyo ilifuzu kwa raundi ya pili baada ya kulaza Mauritius kwa jumla ya 5-2 baada ya kutoka sare tasa mechi ya marudiano jijini Nairobi Jumapili.

Kenya imeorodheshwa nambari 131 na Cape Verde nambari 41.

Ethiopia, waliobandua Sao Tome e Principe watakutana na Congo-Brazaville raundi ijayo.

Mechi za raundi hiyo zitachezwa mwezi Novemba.

Baada ya raundi ya kwanza kuchezwa, kutakuwa kumesalia timu 40 ambazo zitapigania nafasi tano za kufuzu kwa fainali zitakazochezewa Urusi 2015.

Timu 27 bora Afrika wakati wa kufanywa kwa droo miezi mitatu iliyopita mjini Saint Petersburg zilipewa nafuu ya kutocheza mechi za raundi ya kwanza, zikiwemo Algeria na mabingwa wa Afrika Côte d'Ivoire.