Wanaowashambulia Waisrael kuondolewa Jerusalem

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ghasia mjini Jerusalem

Serikali ya Israel imeipa idara ya polisi nguvu zaidi kuzingira kabisa baadhi ya maeneo ya mashariki mwa Jerusalem, kufuatia kuzuka kwa aina mpya ya mashambulio kutoka kwa Wapalestina katika siku za hivi majuzi.

Serikali inasema kuwa utawala nchini humo, pia utabomoa nyumba za Wapalestina wanaowashambulia Waisraeli na kuwapokonya haki ya kuishi mjini Jerusalem.

Askari na walinda usalama wa ziada pia watatumwa mjini humo.

Waisraeli watatu waliuwawa mjini Jerusalem hapo jana Jumanne.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Jerusalem

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani, John Kerry, anasema kuwa atasafiri katika eneo hilo katika siku chache zijazo ili kutuliza ghasia hizo.

Mhariri mkuu wa BBC Mashariki ya Kati, anasema kuwa ni vigumu mno kuwafungia Wapalestina, kwani hii sio mara ya kwanza kwa Israeli kujaribu kuwazingira raia hao.

Kuongezeka kwa ghasia hizo kunafuatia majuma kadhaa ya taharuki katika eneo la msikiti wa Al-Aqsa, maarufu kwa wayahudi kama hekalu la mlimani.