Watanzania wamkumbuka Nyerere mtandaoni

Nyerere
Image caption Watanzania wengi wanatumia mitandao ya kijamii kumkumbuka Nyerere

Watanzania kwenye mitandao ya kijamii wamekuwa wakitumia kitambulisha mada #DearNyerere kumkumbuka mwanzilishi wa taifa hilo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Sikukuu ya Nyerere Dei huadhimishwa kila Oktoba 14 kukumbuka siku aliyofariki kiongozi huyo.

Mwandishi wa BBC Tulanana Bohela anasema Watanzania wamekuwa wakitumia vitambulisha mada kadha kueleza hisia zao kuhusu maono aliyokuwa nayo Bw Nyerere wakati wa uhuru 1961 na hali ilivyo sasa. Mwandishi wetu pia amezungumza na baadhi ya wakazi ambao wanasema mengi ya maono ya Mwalimu Nyerere hayajatimia.

Vitambulisha mada vingine vinavyotumiwa ni #NyerereDay #NyerereDaySpecial na #NyerereQuotes ambapo Watanzania wanakumbuka nukuu muhimu za kiongozi huyo.

Kwa sasa taifa hilo linajiandaa kwa uchaguzi mkuu Oktoba 25, kukiwa na ushindani mkali kati ya chama tawala CCM na muungano wa upinzani Ukawa.

Mwalimu Nyerere alizaliwa Aprili 13, 1922 na akafariki Oktoba 14, 1999.

Aliongoza Tanzania hadi alipostaafu 1985.

Aliendelea kuwa mwenyekiti wa CCM hadi 1990. Alifariki kutokana na saratani aina ya leukemia akitibiwa London.