Mwanaharakati aliyejitolea kubadili mtazamo kuhusu Ukimwi

Phindile Sithole-Spong
Image caption Bi Sithole-Spong aligundua alizaliwa akiwa na virusi vya Ukimwi akiwa na umri wa miaka 19

Phindile Sithole-Spong ni mwanaharakati kutoka Afrika Kusini anayeishi na virusi vya Ukimwi.

Amekuwa akiongoza juhudi za kukabiliana na unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na hususan miongoni mwa vijana.

Mwanamke huyu aligundua akiwa na miaka kumi na tisa kwamba alizaliwa na ugonjwa wa Ukimwi, Phindile alijihusisha na usambazaji wa ujumbe kuhusu Ukimwi na Afya ya Uzazi, hasa maeneo ya kusini mwa Afrika, ambayo yameathirika pakubwa na Ukimwi.

Bi Sithole-Spong, alizindua kampeni ya Rebranding HIV mwaka 2013 kubadili mtazamo wa jamii kuhusu virusi vya Ukimwi, hasa miongoni mwa vijana akiwa katika chuo kikuu cha Cape Town.

Nchini Afrika Kusini takriban asilimia 11.2 ya raia wote wanaishi na virusi vya Ukimwi.

Kwa sasa, Bi Sithole-Spong ni mshauri wa mashirika makubwa ya kimataifa kama vile Muungano wa Afrika na UNAIDS.

Baada ya kufahamu kuwa watu wa rika lake, familia na marafiki walikuwa wameathirika na janga la Ukimwi duniani pamoja na kuongezeka kwa maambukizi mapya nchini Afrika Kusini, licha ya kampeni mbalimbali, Phindile amekuwa akijihusisha na kampeni ya kuendeleza mtazamo chanya kuhusu Ukimwi na Afya ya Uzazi.

''Nina fahari sana moyoni kwa vijana ambao hawaaibiki kuishi na Ukimwi. Sote tunakumbwa na Ukimwi kila siku kama vijana, huwezi kutambua kama mtu ana Ukimwi au la, ni kama tu magonjwa mengine kwa sababu unaweza kujitibu,” anasema.

Kwa harakati zake za kuhamasisha mtazamo mwema kwa watu katika jamii zinazoathirika na janga la Ukimwi, amepongezwa sana.

“Ninafanya kitu ambacho ninakipenda sana. Huwa sihisi kwamba ni kazi. Sijilazimishi. Kwa mfano huwa siandiki hotuba zangu,” anasema.

"Huwa zinatoka katika sehemu halisi moyoni mwangu ambayo ina hamu ya kutaka kusaidia. Ya kutaka kupaza sauti yangu popote inapoweza.”