Jenerali afungwa kwa kushindwa na Boko Haram

Boko Haram Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wa Nigeria wamekuwa wakipiga hatua katika kukabiliana na Boko Haram karibuni

Mahakama ya kijeshi nchini Nigeria imemhukumu kifungo cha miezi sita jela jenerali aliyeongoza wanajeshi walioshindwa vibaya na Boko Haram.

Jenerali Enitan Ransome-Kuti amepatikana na hatia ya kukosa kutekeleza majukumu yake wapiganaji hao wa Kiislamu waliposhambulia mji wa kaskazini mashariki wa Baga, Januari.

Raia wengi waliuawa baada ya Boko Haram kuteka mji huo. Wapiganaji hao pia walifanikiwa kuteka shehena kubwa ya silaha.

Wakili wa jenerali huyo amesema atakata rufaa.

Shtaka jingine la kuwa mwoga liliondolewa.

Idadi hasa ya watu waliouawa wakati wa shambulio hilo mjini Baga bado haijabainika serikali ikidai ni watu 150 waliofariki lakini wenyeji wanadai huenda idadi hiyo ikafika 2,000.

Kando na kuua watu wengi, Boko Haram waliwateka wanawake wengi ambao waliwatumia kama watumwa wa ngono.

Mahakama ya kijeshi mjini Abuja imesema Jenerali Ransome-Kuti alifanya vyema kuwaagiza wanajeshi wake wajiondoe uwanja wa mapigano baada ya kuzidiwa nguvu lakini wakasema alifaa kuitisha usaidizi na kushambulia tena kwa lengo la kuuteka mji huo tena.