Congo:4 Wanaompinga Sassou Nguesso wauawa

Haki miliki ya picha
Image caption Maandamano yameanza nchini Congo kupinga hatua ya rais wa nchi hiyo Denis Sassou Nguesso kuwania muhula wa tatu

Maandamano yameanza nchini Congo kupinga hatua ya rais wa nchi hiyo Denis Sassou Nguesso kuwania muhula wa tatu.

Polisi wa kukabiliana na fujo nchini humo wamefyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi wakijaribu kuvunja maandamano hayo.

Takriban watu wanne wameripotiwa kuuawa katika makabiliano hayo katika mji mkuu wa Congo Pointe-Noire.

Maandamano hayo yameibuka huku ikiwa imesalia mwezi mmoja tu kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni ya kuamua iwapo taifa hilo litafutilia mbali kipengee cha katiba kinachomzuia rais wa taifa hilo kuongoza kwa zaidi ya mihula miwili.

Aidha raia wataamua iwapo rais atakayeongoza taifa hilo anastahili kuwa amezidi umri wa miaka 70 au la.

Rais Sassou Nguesso ana umri wa miaka 72 na kikatiba haruhusiwi kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao kwani amekuwa uongozini kwa zaidi ya awamu mbili.

Ametawala nchi hiyo kwa zaidi ya miaka thelathini sasa.