Zimbabwe yafurahia kina dada kufuzu Olimpiki

Ruth Neshamba Haki miliki ya picha Getty
Image caption Timu za Zimbabwe zimekuwa mara nyingi zikibanduliwa na Cameroon mashindano makubwa

Timu ya taifa ya soka ya kina dada ya Zimbabwe imeandikisha historia baada ya kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki kwa mara ya kwanza kabisa.

Kina dada hao kwa jina - Mighty Warriors – walifuzu kwa michezo hiyo itakayoandaliwa mjini Rio de Janeiro mwaka ujao kwa kulaza Cameroon 1-0.

Bao la Zimbabwe lilifungwa na Rudo Neshamba dakika ya nane.

Neshamba, alikuwa amewafungia bao moja ugenini Yaounde mechi ya mkondo wa kwanza walipolazwa 2-1.

Matokeo kwa jumla yalikuwa 2-2 lakini Zimbabwe wakafuzu kwa kuwa na bao la ugenini.

“Huu ni ufanisi mkubwa sana kwetu. Nina furaha sana. Hata siwezi nikaeleza kwa maneno vile ninavyohisi sasa,” alisema nahodha wa timu hiyo Felistas Muzongondi.

Hii ni mara ya kwanza kwa timu yoyote ya kandanda kutoka Zimbabwe kufika kwa fainali za dimba kubwa la dunia.

Timu za taifa za nchi hiyo zimekuwa zikivunjwa moyo mara kwa mara na Cameroon.

Kwa miaka mingi, taifa hilo limekuwa likibanduliwa kutoka vinyang’anyiro vya kufuzu kwa Kombe la Dunia na Kombe la Taifa Bingwa Afrika na Cameroon.

Mdadisi wa BBC wa masuala ya Afrika Stanley Kwenda anakumbuka mwaka 2004 katika Kombe la Taifa Bingwa Afrika walipobanduliwa na timu iliyokuwa na wachezaji matata kama vile Samuel Eto'o na Patrick Mboma.

Zimbabwe wataungana na Afrika Kusini katika michezo ya Rio 2016 ambao walilaza Equatorial Guinea 1-0 mjini Bata.