Ufugaji wa mbwa ulianza Asia, utafiti waonyesha

Mbwa Haki miliki ya picha Getty
Image caption Watafiti wanakubaliana mbwa wamekuwa wakitumiwa na binadamu kwa miaka 15,000

Utafiti mpya unaonyesha kuwa mbwa walianza kufugwa kwa mara ya kwanza katikati mwa bara Asia.

Watafiti hao walichunguza chembe za msambojeni (DNA) za aina 165 ya mbwa, kutoka mataifa 38 katika kile wanachosema ni utafiti mkubwa zaidi, kuwahi kufanyika duniani kuhusiana na uzao wa mbwa.

Utafiti huo unasema kuwa Nepal na Mongolia ni maeneo ya kwanza kabisa ambapo mbweha walianza kuwa marafiki wakubwa wa binadamu, lakini haijasema ni lini tukio hilo lilifanyika.

Kuna dhana nyingine kuwa mbwa walianza kufugwa kwa mara ya kwanza kusini mwa Uhina, bara ulaya, Siberia, au Mashariki ya Kati, yapata miaka elfu kumi na mitano iliyopita.

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa kwenye toleo la hivi punde la jarida la Proceedings of the National Academy of Sciences, linalochapishwa nchini Marekani.