Wafahamu wagombea wote wanaowania urais Tanzania

ANNA ELISHA MGHWIRA

Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo)

Image caption Mghwira ndiye mwanamke pekee anayewania urais

Ndiye mgombea pekee wa kike kinyang’anyiro cha urais mwaka huu.

Yeye ni mwenyekiti wa chama cha ACT Wazalendo, chama kichanga zaidi Tanzania kilichoundwa 2014.

Mghwira, 56, anatoka mkoa wa Singida. Babake alikuwa diwani na kiongozi chama cha Tanu na baadaye CCM.

Ana shahada ya uzamili katika Sheria (LLM) kutoka Chuo Kikuu cha Essex, UK na shahada ya kwanza katika Theolojia kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini.

Mghwira alijiingiza katika siasa mara ya kwanza kwenye Tanu Youth League lakini baadaye akaangazia masomo na familia. Alijiunga na Chadema 2009 na kushikilia viti kadha vya uongozi ngazi ya wilaya na mkoani.

Alijiunga na ACT – Wazalendo Machi mwaka huu na kuchaguliwa mwenyekiti.

CHIFU LUTALOSA YEMBE

Alliance for Democratic Change (ADC)

Alikuwa awali mwanachama wa Civic United Front (CUF) na mwenyekiti wake Shinyanga. Alijaribu kumuengua mwenyekiti wa CUF Prof Ibrahim Lipumba, lakini akashindwa na mwishowe akatimuliwa chamani.

Yeye yumo kwenye biashara ya madini na ameahidi kuimarisha mambo manne akichaguliwa rais: afya, maji, ukusanyaji wa ushuru na matumizi mema ya rasilimali.

EDWARD NGOYAI LOWASSA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) / Ukawa

Image caption Lowassa alikuwa Waziri Mkuu kuanzia 2005 hadi 2008

Ndiye mgombea mkuu wa upinzani kupitia Chadema (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) moja ya vyama vine vilivyoungana chini ya Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi).

Lowassa, 62, anatoa mkoa wa Arusha na amekuwa mbunge wa Monduli kwa muda mrefu.

Alihudumu kama Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia 2005 hadi kujiuzulu kwake Agosti 2008.

Alikuwa waziri katika wizara kadha: Masuala ya Mahakama na Bunge (1990-1993), Ardhi na Makao (1993-1995), Mazingira na Kukabiliana na Umaskini (1997-2000), Maji na Mifugo (2000-2005).

Ana shahada ya uzamili katika Masomo ya Ustawi kutoka Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza.

Lowassa alijaribu kuwania urais 1995 lakini akachujwa mapema. 2005 alimpigia debe Jakaya Kikwete ambaye aliposhinda, alimteua Waziri Mkuu.

Alisaka tiketi ya CCM wakati huu na alipochujwa akahamia Chadema.

FAHMI NASSORO DOVUTWA

United People Democratic Party (UPDP)

Ndiye mwenyekiti wa United Peoples Democratic Party (UPDP).

Dovutwa, 58, alikuwa mmoja wa walioteuliwa na Rais Kikwete kuwakilisha vyama vya kisiasa kama mjumbe Bunge la Katiba lililokuwa na vikao vyake Dodoma.

Rasimu ya katiba iliyotayarishwa ilizua utata na shughuli hiyo haijakamilika.

Aliwania urais 2010 chini ya UPDP na akashinda asilimia 0.16 ya kura, baada ya kujiondoa dakika za mwisho.

HASHIM RUNGWE SPUNDA

Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA)

Spunda aliwania urais 2010 akitumia NCCR Mageuzi lakini akapata asilimia 0.3 ya kura.

Ni wakili wa Mahakama Kuu anayehudumu kibinafsi.

Anatoka eneo la Ujiji, Kigoma.

Spunda, 66, alikuwa mfuasi sugu wa Tanu na baadaye CCM, na baada ya kuingia kwa siasa za vyama vingi 1992 alisalia chama tawala miaka mingine mitatu kabla ya kujiunga na NCCR Mageuzi 1996.

Aliondoka NCCR Mageuzi 2012 na kuanzisha Chaumma, chama ambacho yeye ndiye mwenyekiti wa kitaifa.

Aliwania ubunge mara mbili bila kufua dafu, 1995 jimboni Kawe na 2005 jimbo la Kinondoni.

JANKEN MALIK KASAMBALA

National Reconstruction Alliance (NRA)

Kasambala ni mfanyabiashara ambaye alikuwa baharia. Aliwahi kufanya kazi na shirika la MV Scorpion kutoka Cyprus nchini Uganda ambako alikamatwa na wanajeshi watiifu kwa Idi Amin Dada alipokuwa akirejea nyumbani baada ya kufanyakazi miezi mitatu.

Alijuiliwa miaka mitatu akishukiwa kuwa jasusi wa Tanzania.

Aliachiliwa baadaye na waliomteka wakamuomba ajiunge nao kupigana dhidi ya wanajeshi wa Milton Obote akiwa Luteni. Alipanda ngazi na kuwa kapteni.

Baadaye alirejea Tanzania na kuanzisha kampuni ya kutemngeneza mitambo na vifaa vya umeme kwa jina Banamoja.

Baada ya kuanza kwa siasa za vyama vingi 1992, pamoja na James Mapalala, walianzisha Civic Movement ambayo mwishowe ilibadilika na kuwa chama cha Civic United Front.

Alikuwa katibu wa chama hicho mkoa wa Ilala na aliwania ubunge jimbo la Ukonga 2005 lakini akamaliza wa tano.

JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI

Chama cha Mapinduzi (CCM)

Image caption Magufuli amekuwa Waziri wa Ujenzi

Ndiye mgombea wa chama tawala na anatoka mkoa wa Geita, kaskazini magharibi mwa Tanzania.

Magufuli, 56, amekuwa mbunge wa Chato tangu 1995.

Amekuwa waziri wa ujenzi tangu 2011. Awali, alihudumu kama Waziri wa Ujenzi (2000-2005) baada ya kuhudumu kama waziri msaidizi wizara hiyo tangu 1995, Waziri wa Ardhi na Makao (2005-2008) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi (2008-2010).

Ana shahada ya udaktari katika kemia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

MACHMILLAN ELIFATIO LYIMO

Tanzania Labour Party (TLP)

Image caption Lyimo anaahidi kutekeleza mabadiliko

Anatoka eneo la Vunjo mkoani Kilimanjaro.

Lyimo, 51, alijiunga na TLP 1999 na akawania ubunge Temeke bila kufanikiwa 2000. Alijaribu tena Arusha 2010 bila kufua dafu.

Ameahidi kufanikisha mageuzi ya kiuchumi na kijamii, akisema watu waliokuwa kwenye mfumo wa kisiasa wa sasa hawawezi kuaminiwa kutekeleza mageuzi hayo.

Ana shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).