Netanyahu atibua hisia kali Palestina

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Netanyahu atibua hisia kali Palestina kuhusiana na mauaji ya kimbari ya wayahudi

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekosolewa baada ya kudai kuwa kiongozi wa kidini mpalestina alimshawishi aliyekuwa kiongozi wa kimla wa Ujerumani Adolf Hitler kutekeleza maauaji ya kimbari ya wayahudi.

Kiongozi mkuu wa kidini mjini Jerusalem Haj Amin al Husseini kwa muda mrefu amekuwa akituhumiwa kuwa anaunga mkono mauaji ya kimbari ya wayahudi.

Lakini katika hotuba yake kwenye mkutano wa kimataifa wa wayahudi, bwana Netanyahu ameendeleza shutuma hizo.

Kulingana naye, Hitler alitafuta maoni kutoka kwa kiongozi huyo wa kidini kuhusiana na ari yake ya kuwafurusha wayahudi barani Ulaya.

Kwa maelezo yake Netanyahu, kiongozi huyo alimwambia Hitler kuwa wayahudi wote wangeenda Palestina iwapo angewafukuza Ulaya.

Na Hitler alipomuuliza,afanye nini ?

Image caption Netanyahu, anasema kuwa kiongozi huyo alimshauri Hitler "awateketeze wayahudi"

Netanyahu, anasema kuwa kiongozi huyo alimshauri Hitler "awateketeze wayahudi"

Wataalam wa maswala ya historia hata hivyo wamekuwa wakipuuzilia mbali madai hayo kuwa siyo ya kweli.

Viongozi wa upinzani nchini Israel wametaja madai ya Netanyahu kama historia ya kupotosha.

Viongozi wa kipalestina kwa upande wao wamesema matamshi hayo yanaonyesha jinsi Waziri huyo mkuu wa Israeli anawachukia wapalestina.