Mwanajeshi wa Israel amuua Mwisraeli kimakosa

Israel Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kumekuwa na ongezeko la mashambulio kutoka kwa Wapalestina Israel

Mwanajeshi wa Israel amemuua raia wa Israel Myahudi kimakosa baada ya wawili hao kukabiliana kila mmoja akidhani mwenzake alikuwa Mwarabu aliyepanga kushambulia, ripoti zinasema.

Mwanamume huyo amepigwa risasi baada yake kujaribu kutwaa bunduki ya mwanajeshi huyo kwenye mfarakano.

Kwa mujibu wa ripoti kwenye vyombo vya habari nchini Israel, mwanamume huyo Mwisraeli aliwakabili wanajeshi wawili wa Israel waliokuwa wakiabiri basi katikati mwa Jerusalem Alhamisi, akidhani walikuwa washambuliaji.

Polisi wanasema wanajeshi hao nao walimshuku mwanamume huyo kuwa mshambuliaji na wakamwitisha kitambulisho chake. Alikataa kutoa kitambulisho na mfarakano ukazuka. Ni hapo ambapo mwanamume huyo alishika bunduki ya mwanajeshi moja lakini akapigwa risasi na kuuawa na mwanajeshi huyo mwingine.

Kisa hicho kimetokea huku wasiwasi ukizidi kupanda kutokana na ongezeko la mashambulio dhidi ya Waisraeli na pia uhasama kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Alhamisi, Wapalestina wawili walipigwa risasi baada ya kumdunga kisu na kumjeruhi Mwisraeli katikati mwa Israel, polisi wanasema.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kerry anakutana na Netanyahu nchini Ujerumani

Hayo yakijiri, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani John Kerry ametoa wito kwa Waisraeli na Wapalestina “kukomesha uchochezi, na kusitisha ghasia”, wakati wa kuanza kwa mashauriano kati yake na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Berlin.

Mazungumzo hayo yanafanyika kabla ya mkutano uliopangiwa kufanyika wikendi kati ya Bw Kerry na kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas nchini Jordan.