Oliseh asema ameshangazwa na uamuzi wa Emenike

Emenike Haki miliki ya picha AFP
Image caption Emenike amechezea Nigeria mechi 37

Kocha wa timu ya taifa ya Nigeria Sunday Oliseh amesema ameshangazwa sana na hatua ya Emmanuel Emenike kustaafu kutoka soka ya kimataifa.

Mshambuliaji huyo wa umri wa miaka 28 alifichua wiki hii kwamba hatachezea tena Super Eagles.

"Niliposikia habari hizo mara ya kwanza niliamua lazima nimpigie simu Emenike anifafanulie yaliyokuwa yakifanyika. Lakini hakupokea simu,” Oliseh ameambia BBC Sport.

"Ninashangaza na kushtua kwa sababu tulifanya kazi pamoja katika mechi zangu za kwanza nne zilizosimamia kama kocha wa Super Eagles."

Oliseh akaongeza: "Yeye alikuwa kwenye sehemu ya mpango wetu wa kuunda upya kikosi na sikuona dalili zozote za kutoelewana au matatizo nikifanya kazi na mchezaji mzuri kama Emenike."

Duru zilidokeza Emenike alikuwa ameachwa nje ya kikosi cha Nigeria kitakachocheza mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia dhidi ya Swaziland mwezi ujao kwa kuwa hajafunga bao lolote ngazi ya kimataifa miaka miwili sasa.

Lakini Oliseh, aliyemrithi Stephen Keshi kama kocha Julai, alisisitiza hakuna ukweli wowote katika madai hayo.

Emenike alichezea taifa hilo mara ya kwanza mechi ya kirafiki dhidi ya Sierra Leone mjini Lagos Februari 2011 na ndiye aliyekuwa mfungaji mabao bora fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika 2013, aliposaidia Nigeria kushinda kombe hilo.

Alichezea Super Eagles mechi 37 na kuwafungia mabao tisa.