Goodluck ahimiza watakaoshindwa wakubali matokeo

Goodluck
Image caption Jonathan alishindwa uchaguzini Nigeria mapema mwaka huu

Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonathan amehimiza tena watakaoshindwa uchaguzini Tanzania wakubali matokeo.

Bw Jonathan, ambaye ndiye kiongozi wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Tanzania kutoka Jumuiya ya Madola, ameeleza matumaini yake kwamba matokeo yatakubalika.

Akizungumza na BBC, kiongozi huyo aliyeshindwa uchaguzini nchini mwake mwezi Machi mwaka huu, amesema watu wanafaa kukubali kwamba uchaguzi ni shughuli ya kidemokrasia na wapiga kura wana haki ya “kuwakubali au kuwakataa”. Bw Jonathan alishindwa uchaguzini na Muhammadu Buhari na akakubali matokeo hayo.

Bw Jonathan amesema amefurahishwa na jinsi kampeni zimeendeshwa akisema zimekuwa za amani.

Kiongozi huyo amekuwa akikutana na wadau mbalimbali kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili Oktoba 25.

“Ninaamini uchaguzi utakuwa huru na wa haki,” amesema.

Ripoti ya awali kutoka kwa ujumbe huo itatolewa Jumanne wiki ijayo na Rais Jonathan anasema anatumai itakuwa "njema”.