Uchaguzi TZ:Polisi wasema wamejiandaa

Image caption Inspekta jenerali wa polisi nchini tanzania Ernest Munga

Inspekta jenerali mkuu wa polisi nchini Tanzania Ernest Munga amesema kuwa maafisa wa polisi wanatarajia kuwepo kwa wasiwasi pamoja na matukio machache ya ghasia kwa kuwa huu ndio uchaguzi ulio na ushindani mkubwa.

Ameyataja maeneo kama vile Dar Es Salaam,Zanzibar,Mtwara,Mwanza,Arusha na Mbeya kama maeneo ambayo huenda yakakumbwa na ghasia na hivyo basi maafisa wengi tayari wametumwa huko.

Anasema kuwa maafisa wa polisi pia watapiga doria katika barabara kuanzia hapo kesho saa kumi na mbili jioni wakati ambapo wanatarajia kwamba mikutano yote ya kisiasa itakuwa imekamilika.

Ameongezea kuwa vituo 65,000 vya kupigia kura nchini kote vitalindwa na polisi mmoja katika kila kituo.

Afisa huyo wa polisi amesema kuwa mkusanyiko wowote wa watu 3 au zaidi watakaoonekana karibu na vituo vya kupigia kura watatawanywa ama hata kukamatwa.

Amethibitisha kwamba baadhi ya wananchi walio na asili za Kihindi wamekuwa wakiondoka nchini lakini anasema kuwa wanafanya hivyo kila wakati wa uchaguzi huku akiongezea kuwa uchaguzi wa mwaka huu ulio na ushindani mkubwa idadi ya watu wanaoondoka imeongezeka.

Pia amethibitisha kwamba baadhi ya raia wamekuwa wakinunua na kuhifadhi vyakula muhimu kwa hofu ya kuzuka kwa ghasia.

Lakini ameongezea kuwa maafisa wake wa polisi wamejiandaa vilivyo.

Katika kipindi cha hivi karibuni kikosi cha polisi nchini humo kilipata magari 399 kati ya 770 waliyohitaji ili kuwawezesha kukabiliana na tatizo lolote.