Wakenya mpakani wasema ‘uchaguzi huu si wa kawaida’

Namanga
Image caption Baadhi ya Wakenya mpakani wameingiwa na msisimko wa uchaguzi Tanzania

Raia wa Kenya wanaoishi katika mji wa Namanga unaopakana na Tanzania wametaja uchaguzi wa Tanzania mwaka huu kuwa wa kihistoria ikilinganishwa na chaguzi za awali nchini humo.

Mji wa Namanga, ulio takriban kilomita 162 kutoka Nairobi, ni miongoni mwa vituo vya mpakani kati ya Kenya na Tanzania vinavyofahamika kwa shughuli za kibiashara kati ya raia wa mataifa hayo mawili.

Eneo hilo pia hushuhudia misafara ya watalii ambao huchangia kuwapa wenyeji wa maeneo hayo mapato.

Ingawa uchaguzi ni shughuli ambayo huja baada ya miaka mitano, safari hii inaonekana kuwavutia raia wa Kenya ambao hawajasita kueleza hali ya jirani.

Wengi wao wakiwemo wafanyabiashra na wakazi wa mji huo, ambao wamekuwa wakitangamana na wenzao wa Tanzania kutokana na ujirani wao, wamesimulia kuwa uchaguzi wa taifa hilo mwaka huu hautabiriki kwani upinzani umekuwa na nguvu zaidi.

''Nimeshuhudia shughuli ya uchaguzi enzi za Mwinyi (Ali Hassan), Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, lakini mwaka huu naona kuna mabadiliko zaidi. Upinzani unatisha kweli,'' Mama Gladys Mami mmoja wa wakazi hao, ameambia mwandishi wa BBC Abdinoor Aden.

Mama huyu amesema kuwa amekuwa akiishi katika mji huo kwa muda mrefu lakini ameshangazwa na hamasa za kampeni.

''Wimbi la kisiasa limenishangaza sana, raia wana hamasa sana,'' ameongeza.

Image caption Baadhi ya magari ya Wakenya wamewekwa nembo za wagombea wa Tanzania

Wakazi wengine mjini Namanga wameeleza kuwa shughuli za uchaguzi zimetatiza biashara kati ya wawekezaji wa Kenya na Tazania.

Mzee Khalif Omar alitoa mfano kuwa kiwango cha mapato na uwekezaji kwenye ushirikiano wake na wenzake kutoka Tanzania kimepungua sana mwaka huu.

Hata hivyo vijana wa Kenya wamechukulia jinsi vijana wa Tanzania walivyoupa uchaguzi kipaumbele lakini wanahisi kuwa wananchi wa jamhuri ya Tanzania watafanya uchaguzi wa amani kutokana na undugu na ukarimu walionao.

''Ni watu wenye busara na undugu. Hatuwezi tukajilinganisha nao. Sidhani kuna haja ya kuwa na wasiwasi, '' alieleza.