Zuma aahidi karo ya vyuo haitaongezwa Afrika Kusini

Zuma Haki miliki ya picha AP
Image caption Zuma amesema kuna mambo kadha yaliyoibuliwa ambayo pia yatashughulikiwa

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma ameahidi kuwa vyuo vikuu havitaongeza ada ya masomo mwaka ujao baada ya wanafunzi wa vyuo hivyo kuandamana kwa wiki moja.

Maandamano hayo ya wanafunzi ndiyo makubwa zaidi kushuhudiwa nchini humo tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi 1994.

Wanafunzi hao awali walikataa pendekezo la serikali la kuweka nyongeza ya ada katika 6%, badala ya kati ya 10% na 12% iliyokuwa imependekezwa na wasimamizi wa vyuo.

Bw Zuma alitangaza hatua hiyo huku mamia ya wanafunzi wakikusanyika nje ya afisi yake.

Kabla yake kuhutubu kupitia runinga, polisi walikuwa wametumia mabomu ya kutawanya waandamanaji kutawanya wanafunzi waliotaka kuingia jengo la Union Building, lenye makao makuu ya serikali mjini Pretoria.

Jumatano, polisi walikuwa wamekabiliana na wanafunzi waliokuwa wakitaka kuingia majengo ya Bunge mjini Cape Town.

Vyuo vikuu kadha tayari vilikuwa vimefungwa kutokana na machafuko hayo.

"Tumekubaliana kwamba karo ya vyuo vikuu haitaongezwa mwaka 2016,” Bw Zuma alisema baada ya kukutana na wakuu wa vyuo na wawakilishi wa wanafunzi.

“Kuna mambo ambayo yamebuliwa mkutanoni ambayo yanahitaji kufuatiliwa zaidi – haya ni pamoja na elimu bila malipo, vyuo kujisimamia na ubaguzi wa rangi.”

Haki miliki ya picha AFP

Wakati wa maandamano hayo, vyuo vikuu vilikuwa vimejitetea na kusema vinahitaji kuongeza karo ili kudumisha viwango vya ubora wa elimu, vikisema vimeathirika na kupunguzwa kwa ufadhili kutoka kwa serikali.

Waandishi wa habari wanasema maandamano hayo yameonyesha wengi wameanza kutofurahishwa na chama tawala cha African National Congress (ANC), kilichoingia mamlakani 1994, hasa kuhusu umaskini, ukosefu wa ajira na ufisadi serikali.

Wengi wa wanafunzi weusi wanasema wametoka familia maskini, na nyongeza ya karo itawazuia kusoma.

Baadhi ya wanafunzi Wazungu pia walijiunga na maandamano hayo, kuonyesha uungaji mkono wao kwa wanafunzi wenzao weusi.