Utafiti: Sauti nzito kwenye kima huficha udhaifu

Kima Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kima dume hutumia sauti nzito kuvutia kima jike

Sauti nzito na kali ya aina ya kima wanaojulikana kwa kupiga kelele huenda huwa ni njia ya kuficha udhaifu kwenye nguvu za uzazi, wanabiolojia wanasema.

Utafiti wa wanasayansi umefichua kwamba wanyama hao hujaliwa sauti kubwa au korodani kubwa, lakini hakuna mnyama anayepata yote mawili.Wanasayansi waligundua hilo walipokuwa wakijaribu kuelewa jinsi nyani hao walianza kutoa sauti na kelele zao.

Matokeo hayo yanaonyesha hali ya kufidia udhaifu katika kiungo kimoja kwa kuimarisha kiungo kingine huenda likawa jambo la kawaida zaidi kuliko inavyodhaniwa.

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa kwenye jarida la kibiolojia la Current Biology.

Kima hao wapiga kelele hutumia kelele zao kufukuza wapinzani na pia kuvutia kima wa kike.

Huwa wamejaliwa mfupa maalum kooni ambao huongeza nguvu kwenye sauti yao. Ukubwa wa mfupa huu kwa jina ‘hyoid bone’ huchangia kima kutoa sauti kubwa.

“Kima wa kike huvutiwa na sauti nzito,” anasema mtafiti mkuu Dkt Jake Dunn kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge.

Anasema baada yao kuchunguza ukubwa wa mifupa hiyo ya kooni kwenye aina mbalimbali za kima, waligundua kuna tofauti kubwa.

“Mfupa mkubwa zaidi ulikuwa na ukubwa mara 14 kushinda mfupa wa kima aliyekuwa na mfupa mdogo zaidi,” anasema Dkt Dunn.

Waligundua pia tofauti kubwa katika ukubwa wa pumbu za kima hao.

Waliokuwa na pumbu kubwa zaidi zilikuwa kubwa mara 6.5 kushinda zile ndogo zaidi.

Haki miliki ya picha Getty

Baada ya kuchunguza kwa kina, Dkt Dunn na wenzake waligundua ni kama kuna hali ya kufidia kati ya kuwa na “sehemu kubwa ya kutolea sauti na pumbu kubwa – za kutoa mbegu nyingi za kiume”.

Kwenye makundi ya kima ambapo wale wa kike ni wengi na wanashindania wale wa kiume, kima dume walikuwa na sauti nzito lakini korodani ndogo.

Katika makundi ya kima wenye dume wengi na hakuna ushindani mkubwa wa kuhitaji kutumia sauti kuvutia kima jike, dume hao walikuwa na sauti zisizo nzito lakini korodani kubwa.

Kuna wanyama wengine kama vile sili wa baharini, wale wenye miili minene huwa na viungo vidogo vya uzazi.

Mwaka 2012 kulikuwa hata na utafiti uliodai wanaume wenye sauti nzito huwa hawawezi kutoa mbegu nyingi za kiume.