Makamu wa rais wa Maldives akamatwa

Maldives Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mke wa Rais Yameen alijeruhiwa kwenye mlipuko uliotokea Septemba 28

Makamu wa rais wa Maldives amekamatwa kuhusiana na jaribio la kumuua rais wa taifa hilo, waziri wa masuala ya ndani nchini humo amesema.

Ahmed Adeeb anazuiliwa na karibuni atashtakiwa kwa uhaini, Umar Naseer amesema kupitia Twitter

Rais Abdulla Yameen alinusurika kifo baada ya boti aliyokuwa akitumia kusafiri hadi mji mkuu akitoka kuhiji Mecca mwezi jana kulipuliwa.

Misukosuko ya kisiasa imekuwa ikiyumbisha Maldives miaka ya hivi majuzi.

Mzozo ulizuka baada ya Yameen kushinda uchaguzi, wapinzani wakisema kulikuwa na udanganyifu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Adeeb amekamatwa baada ya kuwasili uwanja wa ndege

Maafisa wakuu wa polisi walifutwa kazi kutokana na uchunguzi wa mlipuko huo, wiki moja baada ya rais huyo kumfuta kazi waziri wake wa ulinzi.

Polisi wamethibitisha kwamba walimkamata Bw Adeeb akiwa uwanja wa ndege baada yake kurejea kutoka safari ng’ambo.

Bw Yameen hakuumia kwenye shambulio hilo la Septemba 28, lakini mkewe, msaidizi mmoja na mlinzi walijeruhiwa.