Makamu wa Rais wa Maldives akamatwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Makamu wa rais wa Maldives

Makamu wa rais wa visiwa vya Maldives amekamatwa akihusishwa na njama za kutaka kumuua rais wa nchi hiyo, Polisi na maafisa nchini humo wameeleza.

Ahmed Adeeb anashikiliwa na anashutumiwa kuhusika na vitendo vya uhaini, Waziri wa mambo ya ndani Umar Naseer ameeleza kwenye Ukurasa wake wa Twitter.

Rais Abdulla Yameen alinusurika kujeruhiwa baada ya mlipuko kutokea kwenye boti aliyokuwa akiitumia kurejea nyumbani akitokea Uwanja wa Ndege mwezi uliopita.

miaka ya hivi karibuni, visiwa vya Maldives vimekuwa katika mgogoro wa kisiasa.

Usalama umeimarishwa mji mkuu wa Male kukihofiwa kutokea vurugu baada ya kukamatwa kwa makamu wa Rais, Gazeti la Haveeru limenukuliwa.

Asubuhi mapema siku ya jumamosi,malori yakiwa na Polisi na wanajeshi walionekana katika kila mtaa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Maldives alinusurika kwenye ajali ya Boti

Watu wengine watatu walikamatwa jumamosi, akiwemo afisa usalama wa Adeeb na afisa wa kijeshi, shirika la habari la AP limeripoti.

Katika tukio la mlipuko Rais hakujeruhiwa, lakini mkewe na Watu wengine kadhaa walijeruhiwa na mlipuko.

Baada ya mlipuko huo, kulikuwa na tetesi zilizoanza kuvuma kuwa Adeeb alihusika.

Katiba ya Maldives,inamruhusu Makamu wa Rais kumrithi Rais iwapo atakufa,kushindwa kutawala kutokana na ugonjwa au kujiuzulu wadhifa.

Maafisa wamelielezea shambulio hilo kuwa jaribio la mauaji na wamewakamata maafisa wa juu wa polisi wawili wiki moja baada ya Rais kumfuta kazi Waziri wake wa ulinzi.

Bwana Adeeb ambaye amekana kuhusika na shambulio la bomu, amekuwa Makamu wa rais kwa miezi mitatu.

Alichukua nafasi ya aliyekuwa makamu wa Rais ambaye naye alishutumiwa kwa makosa ya uhaini.