Mataifa ‘maskini’ Ulaya yatishia kufunga mipaka

Wahamiaji Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wahamiaji wengi wanataka kwenda Ujerumani

Mataifa ya eneo la Balkan ambayo yamekuwa yakitumiwa na wakimbizi kufikia nchi nyingine za Ulaya wametishia kufunga mipaka iwapo nchi hizo zitakataa kuwapokea wakimbizi zaidi.

Bulgaria imesema itafunga mipaka yake iwapo mataifa yaliyo kaskazini pia yatafunga mipaka yake kuzuia wahamiaji kuingia.

Kauli hiyo imekaririwa na Romania na Serbia pia.

Tishio hilo limetolewa kabla ya kuanza kwa mashauriano kati ya mataifa ya Balkan na mataifa wanachama wa Muungano wa Ulaya.

Rais wa Slovenia amesema taifa hilo litachukua hatua kivyake iwapo hakutapatikana suluhu, kabla ya maji kuzidi unga.

Waziri Mkuu Miro Cerar alikuwa awali amekataa kufutilia mbali uwezekano wa kujenga uzio kwenye mpaka wake na Croatia.

Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) limesema zaidi ya wahamiaji 9,000 waliwasili Ugiriki kila siku wiki iliyopita, idadi ya juu zaidi mwaka huu.

Wengi wa wahamiaji hao, wakiwemo watu wanaotoroka mapigano Syria, Iraq na Afghanistan, wanataka kufika Ujerumani kutafuta hifadhi.

Ujerumani imesema inatarajia kupokea watu 800,000 wanaotafuta hifadhi mwaka huu.

Safari ya wahamiaji hao wanaotaka kuelekea kaskazini imekuwa ikikumbwa na changamoto maeneo ya kusini na mashariki mwa Ulaya, ambako nchi zinasema hazina rasilimali za kuwahudumia.

Mzozo umezidishwa kwa kiwango fulani na hatua ya Hungary kufunga mpaka wake na Serbia na Croatia, na kuwalazimisha wahamuaji kutafuta njia nyingine za kuelekea kaskazini.