Upigaji kura waanza vyema Tanzania

Mwanza
Image caption Katika maeneo mengi tayari foleni ndefu zimeanza kushuhudiwa

Shughuli ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu Tanzania imeanza vyema katika maeneo mengi nchini humo. Wapiga kura walifika vituoni mapema, kila mmoja akitaka kupiga kura kabla foleni hazijakuwa ndefu.

Eneo la Kinondoni, watu walianza kupiga kura bila matatizo yoyote. Sheria ya mita 200 inaonekana kuanza kuheshimiwa kwani watu wanapiga kura na kuondoka vituoni.

Mpiga kura wa kwanza kupata fursa ya kuamua kiongozi wake alisema alifika kituoni saa tisa

Image caption Bwana huyu alikuwa wa kwanza kupiga kura yake Kinondoni

Katika kituo cha Dodoma foleni ndefu imeshuhudiwa ,ni kituo kilichopo katikati ya mji.Baadhi ya wapiga kura waliofika kituoni humo na kupiga kura wanasema hakuna tatizo lolote walilopata.

Mtafarufuku hata hivyo umetokea katika kituo cha Masaki baada ya maafisa wa uchaguzi kutoka nje ya vituo vya kupiga kura na kuwaelezea raia kupanga mistari mitatu inayowapendelea wanawake na wazee.

Wengi wa wale waliofika mapema wamepinga hatua hiyo wakidai kwamba ni haki yao kupiga kura wa kwanza.

Katika eneo la Pasiasi, Mwanza mwandishi wa BBC ABoubakar Famau amekutana na mwanamke mmoja aliyembebea mtoto. Mwanamke huyo anasema kulifaa kuwa na foleni tofauti ya wanawake walio na watoto wachanga.

Image caption Hapa ni kituo cha Pasiasi, kata ya Ilemela, Mwanza

Wapiga kura 22.7 milioni wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo wa leo. Kuna wagombea wanne wa urais wanaotaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete anayestaafu baada ya kuongoza kwa mihula miwili.