Tetemeko kubwa la ardhi latikisa Afghanistan

Tetemeko India Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Tetemeko hilo limetikisa maeneo ya India na Pakistan

Tetemeko kubwa la ardhi limekumba maeneo ya kaskazini mwa Afghanistan, na kutikisa ardhi maeneo ya Pakistan na India.

Kitovu cha tetemeko hilo lenye nguvu ya 7.5 kwenye vipimo vya Richter kilikuwa maeneo yenye milima mingi ya Hindu Kush, kilomita 45 kusini magharibi mwa Jarm, Idara ya Utafiti wa Jiolojia ya Marekani imesema.

Nchini Pakistan, vyombo vya habari vilionyesha picha za watu wakikimbia na kutoka kwenye majengo.

Bado hakuna ripoti zozote rasmi kuhusu majeruhi lakini baadhi ya ripoti zinasema watu wanne wamefariki kaskazini magharibi mwa Pakistan.

Maafisa wanasema tetemeko hilo lilitokea kutoka kilomita 212 ndani ya ardhi. Nguvu za tetemeko hilo awali zimedaiwa kuwa 7.7 lakini baadaye kipimo kikashushwa.

Mwandishi wa BBC katika jiji la Lahore nchini Pakistan anasema mawasiliano ya simu yalitatizika. Wakazi wa mji wa Delhi India walitoka majumbani na kuingia barabarani huku wanafunzi wakiondolewa shuleni.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ameandika kwenye Twitter kwamba ameagiza utathmini ufanywe kuhusu uharibifu uliosababishwa na tetemeko hilo.

Haki miliki ya picha

"Tuko tayari kusaidia iwapo hili litahitajika, hata Afghanistan na Pakistan," amesema.

Eneo hilo hushuhudia mitetemeko mingi ya ardhi inayotokana na mgongano kati ya bara ndogo ya India na maeneo ya kati ya bara Asia.

Mwaka 2005, tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.6 lilikumba maeneo ya Kashmir yanayotawaliwa na Pakistan na kuua watu 75,000.

Aprili mwaka huu, watu 9,000 walifariki na nyumba 900,000 kuharibiwa baada ya tetemeko la ardhi kukumba Nepal.