Mwanamke mjasiriamali anayeangazia chakula cha watoto

Konate
Image caption Marie Konate alianzisha kampuni yake miaka 20 iliyopita

Marie Diongoye Konaté huendesha kampuni pekee ya uzalishaji wa chakula cha kiasili Ivory Coast, akitumia nafaka asilia.

"Hakuna jambo muhimu zaidi maishani kuliko kuwa na mwanzo mwema. Mtu kuwa na utapiamlo akiwa mchanga huathiri sana maisha yake ya baadaye,” anasema.

Hii ndiyo sababu kuu iliyomfanya Marie Konaté kuamua kuangazia vyakula vya watoto wachanga miaka ishiriki iliyopita. Anajivunia kuzalisha chakula asilia, cha bei nafuu na chenye virutubishi tele ambacho kinaweza kutumiwa badala ya chakula cha watoto cha kuagizwa kutoka nje.

Marie Konaté alianzisha kampuni ya Protein Kissèe-La (PKL) miaka 20 iliyopita na ndiye afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo.

"Hii ni biashara ya kilimobiashara inayoangazia uzalishaji wa nafaka ya kutumiwa na watoto na watu wazima, kwa kutumia mazao asilia kutoka mashambani kutoka nchini Ivory Coast.

Kwa sasa anapanga kuanza kutumia mitambo na mashine mpya ili kuimarisha uzalishaji.

“Tunafanyia majaribio mashine na mitambo hii kuona iwapo itatoa chakula cha kiwango cha ubora sawa na mashine zetu ambazo tumekuwa tukitumia awali," anasema

Kwake, anaamini kwamba ni muhimu sana kuwapa watoto lishe bora.

Anasema utapiamlo na umaskini kwa kawaida huanza kuathiri wale wasio na uwezo, watoto.

"Wakilishwa vyema, watoto wao pia watalishwa vyema siku moja. Wakikosa kulishwa vyema wakashiba, hawana uwezo wa kujitoa kutoka kwenye lindi la umaskini siku za usoni,” anaeleza.

Anashangazwa sana na hali barani Afrika ambako mataifa mengi huuza nje ya nchi mazao yanayozalishwa humo na kununua kutoka nje chakula.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Ivory Coast mwaka 2014 iliuza nje bidhaa zinazotoshana na asilimia 43 ya jumla ya pato ghafi la taifa 43% na kuagiza kutoka nje asilimia 39 ya jumla ya pato ghafi la taifa.

Ivory Coast huzalisha takriban 40 ya kakao yote duniani. Lakini chokoleti nyingi madukani nchini humo huagizwa kutoka nje.

“Hili ni jambo linalonishangaza. Mustakabali wetu umo katika kuzalisha vyakula sisi wenyewe Ni ndoto kuamini kwamba tunaweza kutatua matatizo yetu ya utapiamlo na umaskini iwapo hatutaanza kutumia rasilimali zetu wenyewe,” anasema Marie Konaté.

“Tuna wakulima wetu wanaokuza mazao ya kilimo, na utakuwa ni upumbavu kutowasaidia kwa kutumia vitu na bidhaa za humu nchini.

Biashara ya mwanamke huyu ni ndogo sana ukilinganisha na mashirika makubwa ya kimataifa anayoshindana nayo kama vile Nestlé au Danone.

Hana pesa za kulipia matangazo, lakini anasema hana wasiwasi.

"Nilipoamua kuingia katika biashara hii vya vyakula vya watoto, nilidadisi hali ya soko. Upande mmoja una nembo hizi za kimataifa, zinazouzia bidhaa wateja walio na pesa nyingi,” anasema Bi Marie Konaté.

"Na upande ule mwingine kuna maskini, hawana chochote, au chakula pekee walicho nacho ni cha kiasili pekee, kilicho na kiwango cha chini sana cha virutubishi, vitamini, na madini. Na hapo katikati, hakukuwa na chochote. Kulikuwa na pengo. Niligundua mara moja ninaweza kujaza pengo hilo sokoni.”

Baadhi ya vijana huogopa kuanzisha biashara Afrika wakidhani lazima wamhonge mtu fulani ndipo waweze kufanikiwa.

Lakini yeye hakujali hili.

"Nilianzisha biashara hii yangu nikiwa na euro 600 pekee. Ninataka kuwaonyesha kwamba inawezekana. Kufaulu kwangu ni ithibati tosha,” anasema.