Ouattara ashinda uchaguzi Ivory Coast

Ouattara Haki miliki ya picha
Image caption Ouattara amesifiwa kwa kufufua uchumi wa taifa hilo la Afrika Magharibi

Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara amechaguliwa kuongoza taifa hilo kwa muhula wa pili, matokeo ya uchaguzi yanaonyesha.

Kiongozi huyo wa umri wa miaka 73 alishinda uchaguzi huo uliofanyika Jumapili kwa kupata asilimia 83.66 ya kura zote zilizopigwa.

Matokeo ya uchaguzi yanaonyesha zaidi ya nusu ya wapiga kura walijitokeza.

Uchaguzi huo unaonekana na wengi kuwa muhimu sana katika kurejesha uthabiti taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya miaka mingi ya misukosuko ya kisiasa.

Baadhi ya viongozi wa upinzani walikuwa wameota wito kwa wapiga kura kususia uchaguzi huo.

Ouattara, ambaye alitarajiwa na wengi kushinda, anasifiwa kwa kufufua uchumi wa taifa hilo lakini ameshutumiwa kwa kuongoza kwa kiimla na kutoangazia maridhiano.

Mpinzani wake mkuu alikuwa waziri mkuu wa zamani Affi N'Guessan, aliyepata asilimia 9.29 ya kura na alitumia chama cha Ivorian Popular

Front, chake aliyekuwa rais Laurent Gbagbo ambaye Ouattara aliondoa madarakani 2010.

Gbagbo alikataa kukubali kushindwa, na mapigano yakazuka na kusababisha watu 3,000 kuuawa.

Mwishowe aliondolewa mamlakani na vikosi vya Ouattara vikisaidiwa na Ufaransa. Gbagbo kwa sasa anazuiliwa Mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC).

Uchaguzi huo wa Jumapili, ulioshuhudia asilimia 54.63 ya wapiga kura wakishiliki, umesifiwa kuwa huru na wa haki.