Wimbo mpya wa Adele wazidi kuvunja rekodi

Adele Haki miliki ya picha Getty
Image caption Adele amepanga kuzindua albamu mpya mwezi ujao

Wimbo mpya wa mwanamuziki Adele umeendelea kuvunja rekodi, siku chache baada ya kuzinduliwa.

Wimbo huo kwa jina Hello, ambao unarejesha Adele kwenye chati za muziki, uliza nakala 165,000 siku tatu za kwanza.

Mnamo Ijumaa, wimbo huo unatarajiwa kuongoza chati za vibao vya pekee vya muziki Uingereza.

Nyota huyo pia anatarajiwa kuvuma sana Marekani, wimbo huo ukitarajiwa kuwa nambari moja kwenye chati baada ya kupakuliwa mara 450,000 mtandaoni masaa 48 ya kwanza tangu kutolewa kwake.

Video ya wimbo huo, ambayo imeelekezwa na mtengenezaji filamu kutoka Canada Xavier Dolan, kadhalika imevunja rekodi iliyowekwa na Taylor Swift kwa kutazamwa mara nyingi zaidi kwenye mtandao wa Vevo siku yake ya kwanza.

Video ya Hello ilitazamwa mara 27,717,681 Ijumaa iliyopita, na kupita mara wimbo wa Bad Blood wake Swift ambao ulitazamwa mara 20.1 milioni siku ya kwanza baada ya kuzinduliwa mapema mwaka huu.

Video hiyo yake Adele kufikia sasa imetazamwa mara 107 milioni kwenye YouTube.

Mwanamuziki huyo anatarajiwa kuzindua albamu yake kwa jina ‘25’ mnamo Novemba 20.

Adele, ambaye jina lake kamili ni Adele Laurie Blue Adkins ameolewa na ana mtoto mmoja.