Nigeria yatoa picha za washukiwa wakuu wa Boko Haram

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Agosti, Rais Buhari aliwapa wanajeshi makataa ya miezi mitatu kuangamiza Boko Haram

Jeshi la Nigeria limetoa majina ya watu 100 ambao wanadaiwa kuwa viongozi katika kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Boko Haram.

Viongozi wa jeshi wamesema wengi wa watu hao ni viongozi katika kundi hilo.

Mwandishi wa BBC mjini Abuja Chris Ewokor anasema hii ni mara ya kwanza kwa jeshi kutoa picha nyingi za washukiwa wanaosakwa.

Picha hizo 100 zimewekwa pamoja kwenye bango ambalo lilitolewa rasmi kwa umma likiwa na jumbe zilizoandikwa kwa lugha mbalimbali za Nigeria, hasa zinazozungumzwa maeneo yaliyoathiriwa sana na mashambulio ya kundi la Boko Haram.

Jeshi halijasema ni jinsi gani liliweza kuwatambua watu hao lakini picha hizo zinaonekana kutolewa kutoka kwenye video na machapisho yaliyotumiwa kama propaganda na kundi hilo.

Mabango hayo yenye picha hizo pia yana nambari ya simu ya dharura ambazo jeshi limesihi watu kupiga kuwaripoti washukiwa pahala watakapoonekana.

Wanajeshi hao wamesema watasambaza picha hizo maeneo yote ya nchi.

Mwezi Agosti, Rais Muhammadu Buhari alilipa jeshi makataa ya miezi mitatu kulishinda kundi hilo la Boko Haram.

Washambuliaji wa kundi hilo wamekuwa wakitekeleza mashambulio na kuua mamia ya watu. Mamilioni wengine wameachwa bila makao kwenye miaka sita ambayo kundi hilo limekuwa likipigana likitaka kujenga dola ya Kiislamu kaskazini mwa Nigeria.