Phil Collins aamua kurejelea muziki

Phil Collins Haki miliki ya picha AFP
Image caption Collins ni mmoja wa wanamuziki waliofanikiwa zaidi duniani

Mwanamuziki mashuhuri kutoka Uingereza Phil Collins ametangaza kwamba atarejelea uimbaji na kusema hata anapanga ziara ya mataifa mbalimbali duniani.

Kwenye mahojiano na jarida la Rolling Stone, mwanamuziki huyo amesema: “Siko tena katika maisha ya kustaafu. Farasi achatoka nje sasa na yuko tayari kwa mbio.”

Msanii huyo wa umri wa miaka 64, aliyekuwa wakati mmoja kwenye bendi ya Genesis, alitangaza 2011 kwamba alikuwa ameachana na muziki ili kuweza kuwalea na kuwatunza wanawe wawili wa kiume.

Amesema kutokana na mpango uliopo wa kutoa upya nyimbo zake, haitakuwa busara kwake kutotoa nyimbo mpya

Collins hajatoa albamu yoyote ya nyimbo mpya tangu ile ya Testify aliyoitoa mwaka 2002 ingawa aliongoza kwenye chati za muziki mwaka 2010 kwa mkusanyiko wa nyimbo za Motown kwa jina Going Back.

Mwaka 2007, aliumia kwenye ziara ya pamoja ya wanabendi wa Genesis, na kumfanya asiweze kucheza ngoma tena.

Ameambia Rolling Stone kwamba atahamishia studio Miami, Florida na huenda akaanza kurekodi nyimbo mpya mwezi ujao.

Amesema angelipenda sana kutumbuiza katika kumbu Australia na Mashariki ya Mbali.

Collins ni mmoja wa wasanii waliofanikiwa sana, na ni miongoni mwa wanamuziki tatu, pamoja na Paul McCartney na Michael Jackson, waliouza zaidi ya albamu 100 milioni duniani wakiwa kivyao na pia kwenye bendi.

Nyimbo zake maarufu ni pamoja na A Groovy Kind of Love na Against All Odds.

Collins ameshinda tuzo saba za Grammy, sita za Brit, moja ya Oscar na mbili za Golden Globes.