UN yahimiza mataifa kuacha misimamo mikali Syria

Ban Haki miliki ya picha
Image caption Ban ameyataka mataifa kutoangazia sana maslahi ya utaifa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito kwa mataifa kuweka kando misimamo mikali wakati wa mashauriano mjini Vienna kuhusu mapigano yanayoendelea nchini Syria.

Ametoa wito kwa washiriki watano wakuu ambao ni Marekani, Urusi, Iran, Saudi Arabia na Uturuki, kuacha “mtazamo wa utaifa” na kukumbatia “mtazamo wa kutoa uongozi kwa ulimwengu”.

Haya ndiyo mashauriano ya kwanza kabisa kujumuisha Iran, ambayo pamoja na Urusi inamuunga mkono Rais wa Syria Bashar al-Assad.

Marekani na washirika wake wamesisitiza kwamba Bw Assad hawezi kuwa sehemu ya suluhu.

Mapigano hayo yaliyodumu miaka mine Syria yalianza kwa maasi dhidi ya Bw Assad na yamesababisha vifo vya watu 250,000 na watu 11 milioni, ambao ni nusu ya raia wa nchi hiyo, kutoroka makwao.

Image caption Mapigano nchini Syria yalianza 2011

Urusi na Iran majuzi zimezidisha juhudi zao za kijeshi katika kusaidia vikosi vya Assad.

Marekani, Uturuki, Saudi Arabia na mataifa mengine ya Kiarabu Mashariki ya Kati yamekuwa yakisisitiza kwamba Assad hawezi kuchangia katika mpango wowote wa kuamua mustakabali wa Syria.

Mkesha wa mazungumzo hayo, Bw Ban alitoa wito kwa washiriki hao wa tano kuweka kando maslahi yao ya muda mfupi.

“Wanavyozidi kushikilia mitazamo yao ya kitaifa, ndivyo watu zaidi wanavyoteseka na ulimwengu wote utaumia,” alisema. “Kama nisemavyo mara nyingi, hakuna suluhu ya kijeshi.”

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Urusi ilianza mashambulio ya angani Syria mwishoni mwa mwezi Septemba

Waziri wa mambo ya nje wa Sudi Arabia Adel al-Jubeir awali aliambia BBC kwamba Iran sharti ikubali kuondolewa madarakani kwa Assad.

"Ataondoka kupitia mchakato wa kisiasa au ataondoa kwa nguvu,” alisema.

Hayo yakijiri, Waziri wa mashauri ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif alisema mataifa mengine yamegundua hakuwezi kupatikana suluhu bila kushirikisha Tehran.

Mawaziri wa mashauri ya kigeni waliandaa mazungumzo yasiyo rasmi mjini Vienna mnamo Alhamisi, mazungumzo kamili yakitarajiwa kufanyika Ijumaa.