Kifaru asafirishwa kilomita 16,000 akazalishe

Harapan Haki miliki ya picha AP
Image caption Harapan ndiye kifaru pekee wa Sumatra aliyekuwa akiishi nchi za Magharibi

Kifaru dume mmoja amesafirishwa umbali za kilomita 16,000 kutoka Marekani hadi Indonesia ili akazalishe.

Kifaru huyo kutoka Sumatra, ambaye vifaru wa aina yake wamo katika hatari ya kuangamia, amekuwa akiishi katika kituo cha kufugia wanyama pori Marekani.

Mnyama huyo aliyepewa jina la Harapan alizaliwa katika kituo cha kufugia wanyama cha Cincinnati, na ndiye kifaru pekee wa Sumatra aliyekuwa amebaki akiishi katika mataifa ya magharibi.

Wahifadhi wa wanyamapori wanatumai atajamiiana na vifaru jike katika mbuga moja ya kitaifa Indonesia.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Harapan alisafirishwa kwa ndege hadi uwanja wa ndege wa Jakarta

Vifaru wa Sumatra wamo hatarini kutokana na kuharibiwa kwa misitu na uwindaji haramu. Watafiti wanasema wamesalia vifaru chini ya 100 wa Sumatra mwituni.

Harapan mwenye umri wa miaka minane, ambaye jina lake linamaanisha matumaini, alisafirishwa kupitia ardhini, angani na majini hadi hifadhi ya vifaru katika mbuga ya wanyama ya Way Kambas.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Alisafirishwa kwa lori hadi bandarini na mwishowe akabeba na feri hadi Sumatra

Dadake, Suci, aliishi naye katika kituo cha kufugia wanyama cha Cincinnati lakini aliugua na kufariki mwaka jana.

Vifaru wa Sumatra ndio wadogo zaidi na ndio pekee kutoka Asia ambao huwa na pembe mbili. Huwindwa sana na majangili kwa sababu pembe zao hutumiwa kutengeneza tiba ya kiasili Uchina.