Uuzaji wa hisa za MTN wasimamishwa kwa muda

Haki miliki ya picha AP
Image caption Uuzaji na ununuzi wa hisa za kampuni kubwa zaidi barani Afrika ya huduma za simu MTN, zimepigwa marufuku

Uuzaji na ununuzi wa hisa za kampuni kubwa zaidi barani Afrika ya huduma za simu MTN, uliokuwa umesimamishwa kwa muda baada ya kudorora kwa bei ya hisa zake sasa zimeanza kuuzwa.

Soko la hisa la Afrika Kusini JSE lilikuwa limeahirisha biashara ya hisa za kampuni hiyo baada ya hofu kuibuka kampuni hiyo ilipopigwa faini ya dola bilioni 5.2 na serikali ya Nigeria.

Mamlaka ya mawasiliano ya Nigeria iliwatoza faini hiyo kubwa kwa MTN baada ya kuipata na hatia ya kuendelea kuwaruhusu wamiliki wa simu ambazo hazijasajiliwa kuzitumia.

Yamkini serikali ya Nigeria iliudhika sana ilipogundua kuwa watu waliomteka nyara aliyekuwa waziri wa maswala ya uchumi Olu Falae walikuwa wanatumia laini ambayo haijasajiliwa kinyume cha sheria.

Aidha Nigeria ilikuwa inanuia kusitisha mawasiliano ya wanamgambo wa Boko Haram na walaghai ilipotoa amri hiyo laini zote za simu ambazo hazijasajiliwa zizimwe.

Image caption Kampuni hiyo ilipigwa faini ya dola bilioni 5.2 na serikali ya Nigeria

Hatua ya soko la hisa la Afrika Kusini JSE inalenga kuwalinda wenye hisa ambao tayari wamepoteza asilimia 25 % ya thamani ya hisa zao katika kipindi cha juma moja iliyopita.

Kwa sasa afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo, Sifiso Dabengwa, yuko Nigeria akijaribu kutafuta sikio la rais mpya Muhham buhari kuhusiana na swala hilo.

Dabengwa anatarajiwa kuwashawishi maafisa wa Serikali kupunguza faini hiyo kubwa na kuahidi kuwa MTN itafuata masharti yote yaliyowekwa katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika .