Benzema mashakani kuhusiana na ukanda wa ngono

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Benzema mashakani kuhusiana na ukanda wa ngono

Mshambulizi wa Ufaransa Karim Benzema anachunguzwa kufuatia madai kuwa alijaribu kumshurutisha mchezaji mwenza kulipa pesa kwa watu fulani ilikuzuia ukanda wa ngono usichapishwe.

Mshambulizi huyo wa Real Madrid alifikishwa mbele ya hakimu mkaazi wa mji wa Versailles mapema leo baada ya kulala korokoroni.

Polisi wanachunguza iwapo alichangia kwa njia yeyote ya kujaribu kumshurutisha mchezaji mwenza wa Ufaransa Mathieu Valbuena kutoa pesa ilikuwanyamazisha wasaliti waliokuwa wametishia kuchapisha ukanda huo wake wa ngono.

Duru zimeielezea shirika la habari la AFP kuwa tayari mshambulizi huyo wa Real Madrid amekiri kuhusika.

Inaaminika kuwa mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 27 alimshawishi Valbuena kuhusiana na ukanda huo kwa niaba ya rafikiye wa tangu utotoni.

Magazeti nchini Ufaransa yanadai kuwa Benzema alitaja ukanda huo wa ngono walipokuwa katika mazoezi ya mechi ya kimataifa wakiwa Clairefontaine mapema mwezi Oktoba.

Ufaransa ilikuwa ikijiandaa kuchuana na Armenia na Denmark.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Haijabainika iwapo alikuwa akimshauri awanyamazishe wasaliti waliokuwa na ukanda huo wake wa ngono au la .

Haijabainika iwapo alikuwa akimshauri awanyamazishe wasaliti waliokuwa na ukanda huo wake wa ngono au la .

Afisi ya mwendesha mashtaka ya umma imekariri kuwa Benzema anachunguzwa kwa kosa la kushiriki njama ya kumtoza mchezaji mwenza pesa mbali na kujaribu kumshurutisha awalipe wasaliti hao fedha.

Iwapo atapatikana na hatia Benzema huenda akafungwa mwaka mmoja jela.

Aidha haijulikani iwapo madai haya yatamzuia kushiriki katika mechi za kuwania ubingwa wa bara Uropa Euro 2016.