Waziri mkuu Ethiopia:Niko tayari kukosolewa

Image caption Waziri mkuu wa Ethiopia Desalegn

Waziri mkuu nchini Ethiopia ameiambia BBC kwamba haogopi kukosolewa na waandishi licha ya sifa mbaya ya taifa hilo ya ukandamizaji uhuru wa kujieleza.

''Uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu kwa harakati za kidemokrasia na maendeleo'',alisema Halemariam Desalegn.

Alisisitiza kuwa baadhi ya wanablogu na waandishi waliokamatwa mwaka uliopita hawakuwa waandishi na kwamba walihusika na ugaidi.

Mashtaka ya ugaidi dhidi waandishi hao wanaojiita wanablogu wa awamu ya tisa yametupiliwa mbali.

Watano kati yao waliachiliwa mnamo mwezi Julai baada ya zaidi ya mwaka mmoja jela kabla ya ziara ya rais wa Marekani Barrack Obama ,huku wengine wanne wakiachiliwa huru na mahakama moja mwezi uliopita.

Mitandao hiyo ya Zone 9 ilichapisha habari za kuikosoa serikali.

Hatahivyo bwana Desalegn amesema kuwa sio kazi zao zilizowasababisha kukamatwa bali ushahidi unaowahusisha na makundi yanayotaka kuidhoofisha serikali.

''Tuko tayari kukosolewa na waandishi kwa kuwa tunajua kwamba hatuko kamili''.