Obama atoa onyo kali kwa Afrika Kusini

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Barack Obama

Rais wa Marekani Barack Obama ameipa Afrika ya Kusini siku 60 kuondoa vikwazo ilivyowekea bidhaa za kilimo kutoka Marekani la sivyo ataiondolea msamaha wa kodi wa bidhaa zake.

Mpango huo utaathiri bidhaa za Afrika Kusini za karibu $100 milioni kutoka taifa hilo ambazo husafirishwa hadi nchini Marekani.

Bw Obama amechukua hatua hiyo baada ya Afrika Kusini kuendelea kuweka vikwazo kwa wafanyabiashara wa Marekani wanaotaka kuingiza nyama ya kuku nchini humo. Aidha, Marekani inalalamika kwamba Afrika Kusini imekuwa ikiweka vikwazo vingine mbalimbali kwa bidhaa za kilimo kutoka Marekani.

Afrika Kusini ilipiga marufuku uagizaji wa bidhaa za kuku mwezi Desemba kutokana na kutokea kwa mkurupuko wa ugonjwa wa homa ya ndege.

Kwa miaka kadhaa imekuwa ikitoa adhabu ya kodi kwa baadhi ya bidhaa za kuku kutoka Marekani.

Afrika ni moja ya mataifa ya Afrika yanayonufaika kutokana na mkataba wa AGOA ambao huruhusu nchi za bara la Afrika kuingiza bidhaa nyingi Marekani bila kutozwa ushuru.

Mataifa 41 hufaidika kutokana na mkataba huo, lakini kutokana na ukubwa wa uchumi wake, Afrika Kusini ndiyo inayonufaika zaidi.