Wenger amsifu sana kipa Petr Cech

Cech Haki miliki ya picha PA
Image caption Cech alikaa miaka 11 Chelsea kabla ya kuhamia Chelsea

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger amemlimbikizia sifa golikipa wake Petr Cech na kusema ni mmoja wa "magolikipa stadi zaidi kuwahi kuchezea soka Uingereza”.

Cech, 33, alijiunga na Gunners kutoka Chelsea kwa £10m mwezi Juni na amemaliza mechi nane bila kufungwa bao, tatu zikiwa kati ya nne za karibuni zaidi Ligi ya Premia.

Aidha, amezima asilimia 84 ya makombora ya kulenga goli, kiwango cha juu zaidi kushinda kipa mwingine yeyote anayecheza ligi kuu Uingereza.

“Ni kipa mwenye kipaji adimu,” amesema Wenger ambaye vijana wake wanajiandaa kuchuana na Tottenham Jumapili.

"Na si ustadi wake pekee, ni mchezaji mwenye kujitolea na asiyeshusha kiwango. Amejitolea sana katika majukumu yake.

“Ni mmoja wa makipa stadi zaidi kuwahi kuonekana hapa nchini.”

Licha ya kujikwaa mechi zake za kwanza Arsenal, amegeuka nguzo kuu na kuwaokoa sana mechi za karibuni.

Cech anashikilia rekodi ya kukamilisha mechi nyingi bila kufungwa Ligi ya Premia, baada yake kupita rekodi iliyowekwa na kipa wa zamani wa Liverpool, Portsmouth na Manchester City David James ya jumla ya mechi 169 wakati wa ushindi wao wa 3-0 mwezi jana dhidi ya Manchester United.

Cech amekamilisha mechi 172 bila kufungwa ligi kuu, na Wenger anaamini ana miaka mingine mitano hivi ya kung’aa.

"Anacheza katika nafasi ambayo umri huwa si shida sana,” amesema Wenger, akionekana kulinganisha kazi ya kipa na wachezaji wa ndani ya uwanja.