Mwanamume mwenye jina sawa na Taylor Swift

Swift
Image caption Bw Swift anasema huwa anatumiwa barua zinazofaa kwenda kwa mwanamuziki huyo

Mwanamume mmoja nchini Marekani amekuwa akikabiliwa na wakati mgumu kutokana na hali kwamba ana jina sawa na mwanamuziki mashuhuri ya nyimbo za pop Taylor Swift.

Mwanamuziki huyo ambaye pia ni mwigizaji, hujulikana kutokana na vituko vyake vya mavazi na unenguaji kiuno.

Mwanamume huyo anasema ni miaka kadha sasa tangu atambue kwamba kulikuwa na mwanamuziki mwenye jina sawa na lake.

“Sikudhani ni jambo kubwa, ‘Naam, anaimba muziki aina ya country, ni jambo njema. Anajiandikia nyimbo zake, ni vyema sana!'"

Lakini mambo yalibadilika sana kwake baada ya mwanamuziki huyo kupata umaarufu.

Image caption Swift ni mwanamuziki na mwigizaji mashuhuri

Kila aendako, watu huajabia jina lake. "We...unataka kusema jina lako halisi ni Taylor Swift?"

"Hili hufanyika mara nyingi sana kila siku,” Taylor, anayetoka Seattle ameambia kituo cha televisheni cha KOMO 4.

"Hata katika Starbucks (mgahawa uuzao kahawa) hushangaa na kufanya mzaha, ‘Jina lako ni Taylor? Si inaweza kufurahisha sana iwapo jina lako la pili lingelikuwa Swift'.

"Ha, hii hapa kadi yangu. Ha, ha, wanashangaa.”

Taylor anasema wakati mwingine hupokea barua kutoka kwa mashabiki wa Swift mwanamuziki.

Baadhi ya barua husema: "Wewe ni mrembo na mtu mzuri sana. Huwa naimba nyimbo zako kila wakati.”

Mwanamume huyo anasema alilazimika kubadilisha anwani yake ya barua pepe kutokana na usumbufu.

Lakini licha ya matatizo hayo yote, Taylor anasema bado analipenda jina lake.