Mnigeria atwaa ubingwa wa dunia wa Scrabble

Image caption Mnigeria atwaa ubingwa wa dunia wa Scrabble

Raia mmoja wa Nigeria ameushangaza ulimwengu wa mchezo wa kujenga maneno ya Kizungu, Scrabble, kwa kumshinda Mwingereza na kuibuka bingwa wa dunia.

Wellington Jighere, 32, aliweka historia kwa kuwa Mwafrika wa kwanza kushinda mashindano hayo.

Jighere alijenga maneno yenye alama nyingi kama; mentored, avouched na fahlores, yaliyomwezesha kumpiku mpinzani wake Lewis Mackay kutoka Uingereza katika fainali hizo zilizoandaliwa mjini Perth nchini Australia

Jighere alimshinda MacKay 4-0. Licha ya uchovu, aliandika majina magumu kama vile ironists, ungifted, felty, Dacoit, Katti, Yow na Aah.

Image caption Jighere mwenyewe amesema alihisi kana kwamba ''bara la Afrika lilikuwa linamuunga mkono katika fainali hiyo''

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amempongeza Jighere kwa kuipeperusha bendera ya taifa lake vyema.

''Umeiletea sifa Nigeria,'' alisema Rais Buhari

Jighere mwenyewe amesema alihisi kana kwamba ''bara lote la Afrika lilikuwa linamuunga mkono katika fainali hiyo''.

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa Facebook Jighere amesema anashangaa aliwezaje kuibuka kidedea huku akisema kuwa hajakuwa akipata usingizi vyema katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amempongeza Jighere kwa kuipeperusha bendera ya taifa lake vyema

Raia huyo wa Nigeria alicheza mechi 32 katika kipindi cha siku nne kabla ya kushinda katika fainali hizo.

Aidha yeye pamoja na timu nzima ya Nigeria walifika mjini Perth Australia siku moja kabla ya mashindano hayo baada ya kustahimili safari ya saa 20 angani.

Jighere alipigiwa simu na Rais Buhari kufurahia ushindi wake.

Image caption Timu ya Nigeria ilifika Perth siku moja kabla ya Mashindano

Kufuatia ushindi huo Jighere ambaye hana kazi alituzwa dola $10,000 za Marekani.

Rais wa shirikisho la mchezo huo la Nigeria Sulaiman Gora ameiambia BBC kwa njia ya simu kuwa Jighere ni mtu mnyamavu sana na kuwa ''uwezo wake mkuu ni unyenyekevu''.