Shabiki aruhusiwa kutazama filamu mapema

Image caption Madaktari walisema Julai kwamba Fletwood alikuwa amesalia na miezi miwili ya kuishi

Shabiki sugu wa filamu za Star Wars amepewa fursa ya kutazama filamu mpya ya msururu huo wa filamu kwa jina The Force Awakens, wiki sita kabla ya filamu hiyo kuzinduliwa.

Kwenye ujumbe katika Facebook, mkewe Daniel Fleetwood, Ashley, amesema mwanamume huyo wa umri wa miaka 31, ametimiziwa ndoto yake kuu maishani.

Bw Fleetwood, anaugua saratani na aliambiwa na madaktari mwezi Julai kwamba alikuwa amesalia na miezi miwili pekee ya kuishi.

alipewa fursa hiyo baada ya kampeni iliyoendeshwa katika mitandao ya kijamii ikiwa na kitambulisha mada#ForceForDaniel, ambapo raia walitoa wito kwa waandalizi wa filamu hiyo wamruhusu Daniel, anayeugua saratani, kutazama filamu hiyo mapema.

Waigizaji wawili wa Star Wars, Mark Hamill aliyeigiza kama Lke Skywalker na John Boyega anayeigiza kama Finn kwenye filamu hiyo mpya, ni miongoni mwa walioshiriki kwenye kampeni hiyo.

Familia ya Fleetwood ilipigiwa simu na mwelekezi wa filamu hiyo JJ Abrams kufahamishwa kwamba ombi lao lilikuwa limekubaliwa.

Maafisa wa Disney walisema Alhamisi kwamba Fleetwood alitizama filamu hiyo na “wote waliohusika walifurahi sana kwa kufanikisha hilo.

Mark Hamill, aliyeshiriki kwenye kampeni hiyo katika mtandao wa kijamii aliandika baadaye kwamba alijawa na “furaha isiyo na kifani”.

"Nikipata fursa ya kutazama filamu hiyo, huenda hata nikafariki kutokana na furaha,” Daniel alikuwa ameambia jarida la People mapema wiki hii.